October 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mpango kuimarisha huduma watu wenye ulemavu uko mbioni

Spread the love

SERIKALI ya Tanzania kwa kushirikiana na wadau wa sekta binafsi, inaandaa mpango wa taifa wa kuimarisha huduma kwa watu wenye ulemavu nchini. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Hayo yamesema leo Jumatano tarehe 20 Mei 2020 bungeni jijini Dodoma, na Waziri Mkuu wakati akijibu swali la Mwatum Haji, Mbunge Viti Maalum (CCM), aliyetaka kujua mkakati wa serikali katika kuhakikisha huduma za watu wenye ulemavu, zinazingatiwa.

Katika swali lake alilouliza kwa njia ya mtandao na kujibiwa vivyo hivyo, Mwatum amesema kumekuwa na utekelezaji mdogo wa huduma za watu wenye ulemavu kwenye shughuli za kijamii, ikiwemo majengo, vyombo vya usafiri pamoja na vyombo vya habari.

Akijibu swali hilo, Waziri Mkuu amesema mpango huo wa kuimarisha huduma kwa watu wenye ulemavu, utaanza kutumika katika mwaka wa fedha wa 2020/21 hadi 2023/24.

“Lengo la kuanzishwa kwa mpango huo, ni kuimarisha mazingira ya upatikanaji na ufikiwaji wa huduma mbalimbali za jamii, yenye kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu ikiwemo elimu, afya, hifadhi ya jamii, usafiri, barabara, michezo, burudani, vifaa Saidizi, marekebisho, taarifa na mawasiliano,” amejibu Waziri Mkuu.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu amesema Serikali imeweka mwongozo wa utoaji vibali vya ujenzi na usimamizi wa ukaguzi wa majengo kwenye mamlaka za serikali za mitaa wa mwaka 2017, ambao unazingatia mahitaji ya walengwa.

Kuhusu vyombo vya habari kuzingatia mahitaji ya watu wenye ulemavu, Waziri Mkuu amesema Serikali ilifanya mapitio ya Kanuni za Maudhui ya Vyombo vya Habari za mwaka 2011, zinazotaka vyombo vyote vya habari kuwa na wakalimani wa lugha za alama.

“Serikali inaendelea kufuatilia suala hili ili kuhakikisha kuwa vyombo vyote vya habari vinatekeleza agizo hili,” amesema Waziri Mkuu.

error: Content is protected !!