July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mpangaji vurugu ajiandae kupelekwa ICC – Tume

Spread the love

MTU yeyote, awe mpigakura, mwanasiasa mgombea kura na wapambe wake au mwandishi wa habari, atakayebainika kupanga vurugu na kuvunja sheria hivyo kuwa chanzo cha ghasia wakati na baada ya uchaguzi, atastahili kushitakiwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Makosa ya Jinai (ICC). Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Tamko hilo limetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora Tanzania, Bahame Nyanduga katika hotuba ya uzinduzi wa Ilani ya Uchaguzi ya asasi za kiraia (AZAKI) kwenye ukumbi wa Millenium Tower, Kijitonyama, Dar es Salaam.

Nyanduga ambaye ni mwanasheria amesema kupanga vurugu na kuvunja sheria ni mambo yanayochochea uvunjaji wa haki za binadamu, msingi hasa wa mashitaka mbele ya mahakama hiyo ambayo Tanzania imesaini mkataba wa kuanzishwa kwake.

AZAKI zimeandaa Ilani mahsusi ambayo ni muongozo kwa vyama vya siasa na wagombea katika kuomba ridhaa ya kuongoza taifa.

Nyanduga amesema tayari kuna viashiria vya uvunjifu wa amani ikiwemo kuwepo vikundi vya ulinzi vya vyama vya siasa kinyume na Katiba.

Ametaja viashiria vingine kuwa ni kauli zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa ambazo zinaelekeza kutokea kwa matendo yaliyo kinyume cha sheria na taratibu wakati wa uchaguzi.

Baadhi ya kauli ametaja ile iliyotolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Nape Nnauye, ya kwamba chama chao kitapata ushindi ikibidi hata kwa “goli la mkono.”

Kauli nyingine ni “tukiibiwa kura patachimbika,” “ushindi ni lazima,” “serikali haitolewi kwa vikaratasi,” “tutapata ushindi wa tsunami” na “ushindi saa nne asubuhi.”

“Tunashuhudia matukio ya matumizi ya lugha zisizo na staha katika kampeni zinazoendelea nchini. Tume inawakumbusha wanasiasa na wafuasi wao kuzingatia maadili ili kudumisha siasa safi, amani na utulivu wa nchi.”

Amesema kwa kuwa Tanzania ni mwanachama wa Mkataba wa Roma ulioanzisha ICC kupitia mwamvuli wa Umoja wa Mataifa, ieleweke vema kwamba yakitokea makosa yanayotajwa na mkataba huo wakati au baada ya uchaguzi mkuu Tanzania, watakaothibitika kuyatenda, ndio watakaoshikwa na kushitakiwa katika mahakama hiyo kwa makosa ya uchochezi au kupanga njama hizo.

“Kwa nafasi yangu kama mwanasheria niliyehusika katika kesi inayohusu mauaji ya halaiki ya nchini Rwanda katika Mahakama ya Mauaji ya Kimbari nchini Rwanda (ICTR) jijini Arusha, na nimekuwa mdau wa masuala ya ICC, napenda kutoa indhari kwamba viongozi wote watakaochochea vurugu, wawe ndani au nje ya serikali, raia wa kawaida au waandishi wa habari, watachukuliwa hatua.

“Wale watakaodhihirika kutumia lugha za uchochezi ama kushiriki kupanga vurugu na uvunjifu wa haki za binadamu, kwa kiwango ambacho kitailazimu ICC kuchunguza makosa hayo hapa Tanzania, waweza kufikishwa mbele ya mahakama ya ICC,” amesema Nyanduga.

Katika kuhakikisha haki inatendeka wakati wa uchaguzi mkuu, Nyanduga amehimiza Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), kuhakikisha taratibu za uchaguzi zinaendeshwa kwa uwazi, haki, kwa misingi ya sheria na pia wasimamizi wa uchaguzi wasijaribu kuingiza ushabiki wala hi sia binafsi.

error: Content is protected !!