July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Moto wawaka KKKT

Spread the love

WAKATI Asime Modern Mwakilima, Muumini wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Mashariki na Pwani akitafakari kuhama Ukristo na kuingia Uislam, waraka uliosambaza ndani ya kanisa hilo unaelekeza kumtumikia Mungu na si mwanadamu, anaandika Josephat Isango. 

Kumekuwepo na mvutano ndani ya kanisa hilo baada ya taarifa za kumuhusisha Askofu Alex Malasusa kujihusisha kingono na mke wa mtu ambaye muumini wa kanisa hilo.

Kuhusu fikra za kuhama dini Mwakilima amesema, anafikiria kufanya hivyo ili aweze kupata nafuu ya kiroho kutokana na mkwazo anaouona ndani ya KKKT katika kutetea dhambi za viongozi wa kanisa hilo.

Akizungumza  na mwandishi wa habari hii ndani ya ofisi za MwanaHALISI Online amesema, amekwazika kiimani kutokana na mdogo wake Venance Mwakilima kuingizwa kwenye matatizo kwa sababu ya uhusiano wenye shaka kati ya mke wake Leoita Ngoyi na Dk. Malasusa.

“Suala la imani ni langu mwenyewe na Mungu, lakini katika hili naona kiongozi wetu ametumia nguvu nyingi.

“Anamtisha mdogo wangu kwa kila namna sasa huyo shemeji hakai na familia, wamempangia nyumba na anamshitaki mume wake,” anasema Mwakilima na kuongeza;

“Kanisa letu badala ya kusimamia ukweli, kwa sasa limeamua kukandamiza kabisa, wametumwa watu watatu Mzee anayeitwa Kaduma, mama Rweyemamu na Kanali mmoja wa jeshi ambaye hataki kutaja jina lake.

“Wanafika wanataka kujifungia na mdogo wetu kumkandamiza kwa masuala ya kulinda mtu mmoja tu, sisi wana familia haturuhusiwi, tunafukuzwa kama tulivyofukuzwa Muhimbili tusisikilize kinachoendelea.”

Amesema, alitegemea viongozi wa kanisa watajiuliza juu ya anayelalamika pia kuripoti kituo cha polisi na kupewa WH/RB/3334/2015.

Pia amesema, wangehoji kwanini gari iliyotumika kutorosha watoto wa ndugu yake ni ya mfanyakazi wa karibu na kiongozi wa dini, mwenye gari aina ya RV4, yenye namba za usajili T.632 DFT ya rangi ya bluu.

Aaaanasema kuwa, mpaka sasa bado inaaminishwa kuwa habari hii inahusu kanisa na watu wanaitwa wakasali kumwombea mtu ambaye kwenye maombi hafiki.

“Kwani kanisa linaendesha gari?. Bado hatujataja mengi wanachokoza, nahamia Uislamu niseme sasa, maneno haya nimemwambia hata Kaduma na msafara wake waliosema wametoka Luther House kuja kwetu ingawa wanatubagua ili wafanikiwe mkakati wao,” amesema na kuongeza;

“Hajawahi kujiuliza mwandishi kapata wapi majina ya Sijenuna Venance Mwakilima, mwenye hati ya kusafiria Na. AB 524934, Stephania Venance Mwakilima Na. AB 524933, Simon Venance Mwakilima Na. AB 599057 na mama yao Leita Ngoyi Mwakilima Na. AB.524932. ambazo zilisababisha tufungue kesi kuzuia wasisafiri nje ya nchi.”

Uamuzi wa Mwakilima kutaka kukimbilia dini nyingine unakuja siku chache baada ya kuvuja kwa waraka ulioadaiwa kuandikwa na Mchungaji Modestus Lukonge kwa wachungaji wengine 61 wa Dayosisi ya Mashariki na Pwani.

Waraka huo unawataka watafakari upya wito wao katika tuhuma hizo binafsi kwa kiongozi wa kanisa.

Waraka unatajwa kuwa ni wa Lukonge, unanukuu Yoh 8:31-34 “Ninyi mkikaa katika neno langu, mmekuwa wanafunzi wangu kweli kweli; tena mtaifahamu kweli, nayo hiyo kweli itawaweka huru.

“Wakamjibu, Sisi tu uzao wake Ibrahimu, wala hatujawa watumwa wa mtu wakati wo wote; nawe wasemaje, Mtawekwa huru?  Yesu akawajibu, Amin, amin, nawaambia, Kila atendaye dhambi ni mtumwa wa dhambi.”

Pia waraka huo umenukuu Mithali 6:32, na Rom 12:1-2,9 inayosema “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.

“Wala msiifuatishe namna ya dunia hii; bali mgeuzwe kwa kufanywa upya nia zenu, mpate kujua hakika mapenzi ya Mungu yaliyo mema, ya kumpendeza, na ukamilifu. Pendo na lisiwe na unafiki lichukieni lililo ovu, mkiambatana na lililo jema.”

Waraka huo umemalizia kwa maneno “imetupasa kumwogopa Mungu kuliko wandamu. Heri mahangaiko kwa ajili ya Yesu kuliko Maghorofa yanayovunwa kwa unafiki”.

MwanaHALISI limemtafuta Lukonge ili aeleze nia ya kuandika waraka huu kwa wachungaji wenzake bila  mafanikio, ingawa hatua za kumtafuta zinaendelea.

Mchungaji mwingine ambaye hatatajwa kwa hatua ya sasa alikiri kupokea waraka huo na alipoulizwa Lukonge ni nani, amesema anamfahamu kuwa ni mchungaji katika kanisa, Mwanasheria aliyesomea Chuo Kikuu cha Dar es Salaam na Mwanateolojia wa Chuo Kikuu cha Makumira.

error: Content is protected !!