WATU zaidi ya 53 wamefariki duniani huku wengine zaidi ya 100 wakiripotiwa kupotea katika kisiwa cha Maui jimbo la Hawaii nchini Marekani kutokana na moto mkubwa ulioibuka katika msitu wa kisiwa hicho. Anaripoti Mlelwa Kiwale, TUDARCo kwa msaada wa Mitandao ya Kimataifa…(endelea).
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kituo cha polisi cha mji huo wa Maui, imeeleza kuwa moto huo ambao umechochewa na mazingira ya kisiwa hicho kulingana na uwepo wa hali ya kipupwe na ardhi yenye majani makavu, umetajwa kuzidi kuenea katika maeneo mbalimbali ya kisiwa hicho.
Taarifa hiyo iliyolewa leo tarehe 11 Agosti 2023, pia umetajwa kuharibu nyumba, shule, hospitali na maeneo mengine ikiwamo mji wa Lahaina ambao umeathiriwa kwa zaidi ya asilimia 80.
Imeeleza kuwa zaidi ya watu 11,000 wamekosa umeme katika makazi yao kutokana na moto huo uliozuka usiku wa kuamkia jana Alhamisi.
Hata hivyo, jeshi la uokoaji linazidi kufanya jitihada za kuuzima moto huo huku wakazi wa miji hiyo pamoja na watalii wakilazimika kujitosa baharini ili kuokoa maisha yao.
Aidha, Rais Joe Biden ameeleza kusikitishwa na maafa hayo yanayoendelea katika kisiwa hicho na kusema; “Kila mmoja aliyepoteza wapendwa wao na makazi yao watapewa msaada wa haraka,” amesema Rais Biden.
Hawaii huwa inakubwa na moto ambao mwaka 2018 maafa hayo yalitokea tena, pia mwaka 2014 moto huo ulidaiwa kusababisha vifo na kuharibu hekari 2000, magari 31.
Leave a comment