May 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Moto K’koo: Masoko, sehemu za mikusanyiko kukaguliwa

Spread the love

 

SERIKALI ya Tanzania, imeagiza wakuu wa mikoa (RC) kwa kushirikiana na Jeshi la Zima Moto na Uokoaji katika meneo yao, kufanya ukaguzi katika masoko na maeneo ya mikusanyiko ya watu, ili kubaini yenye dosari kwa ajili ya kudhibiti majanga. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).

Agizo hilo limetolewa leo Jumatatu, tarehe 12 Julai 2021 na Waziri wa Mambo ya Ndani, George Simbachawene, alipotembelea Soko Kuu la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, kwa ajili ya kukagua shughuli za uzimaji moto katika jengo la soko hilo.

Sehemu ya juu ya jengo la soko hilo, liliungua usiku wa Jumamosi, tarehe 10 Julai 2021. Ambapo shughuli za uzimaji moto huo zinaendelea kufanywa na jeshi hilo.

Simbachawene amesema, tukio la soko hilo kuungua moto, liwe fundisho na tahadhari katika maeneo mengine.

“Kwa hiyo, kuna maemeo mengi kuna changamoto nyingi, nafikri hatuwezi kurudi tena kwenye maisha yale yale bila ya hizi changamoto kuzidhughulikia.”

“Nawaagiza wakuu wa mikoa wote na kamati za ulinzi na usalama za mikoa, nchi nzima watumie jeshi la zimamoto wapite maeneo yote ya umma, maeneo kama masoko, stendi na yanayojaza watu wengi,” amesema Simnachawene.

Waziri huyo amesema”lazima tuhakikishe tunayalinda kwa kuzingatia mahitaji ya zima moto majanga yanapotokea. Sina hakika kama katika masoko, stendi zetu kuna miundombinu ya kutosha. Hili liwe fundisho.”

Simbachawene amesema, masoko mengi yanakabiliwa na changamoto za miundombinu ya kudhibiti majanga, ikiwemo maji ya kutosha na njia za kupita wakati yanapotokea.

Tayari Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa ameunda tume ya kuchunguza chanzo cha moto huo, ambayo imepewa siku saba kuanzia jana Jumapili hadi Jumapili tarehe 18 Julai 2021, kutoa ripoti kuhusu tukio hilo.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Amos Makalla, wafanyabiashara zaidi ya 200 wameathirika na tukio hilo, ambao walikuwa na vizimba katika soko hilo.

error: Content is protected !!