SERIKALI ya Tanzania imesema, wafanyabiashara takribani 224, wameathirika na tukio la Soko Kuu la Kariakoo, jijini Dar es Salaam, kuungua moto. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam…(endelea).
Taarifa hiyo imetolewa jana Jumapili, tarehe 11 Julai 2021 na Waziri Ofisi ya Rais-Tamisemi, Ummy Mwalimu, siku moja baada ya tukio hilo kutokea usiku wa Jumamosi, tarehe 10 Julai 2021.
Kupitia ukurasa wake wa Twitter, Ummy alisema taarifa za awali zinaonesha baadhi ya mali za wafanyabishara hao zimeibiwa.
Hata hivyo, Ummy alisema wizara yake inasubiri taarifa ya uchunguzi wa tume iliyoundwa na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kuhusu tukio hilo.
Soma zaidi:-
-
Moto soko la Kariakoo: Rais Samia atoa pole, maagizo
-
Majaliwa akagua soko la Kariakoo, atoa siku saba
“Pole nyingi kwa wafanyabiashara wa Soko Kuu la Kariakoo waliokumbwa na janga hili.”
“Tunasubiri taarifa ya uchunguzi ya tume ya waziri mkuu. Taarifa zetu za awali ni kuwa, wafanyabiashara 224 ni wahanga wa janga hili.”
“Pia tumepokea taarifa, kuna wengine mali zao zimepotea au kuibiwa,” aliandika Waziri Ummy.
Aidha, Ummy alisema Serikali itahakikisha masoko yanayomilikiwa na halmashauri, yanakuwa na miundombinu ya kukabiliana na majanga ya moto, ikiwemo kuchimba visima vya maji.
“Masoko yote yanayomilikiwa na halmashauri zetu, hususani masoko makubwa, stendi zetu zote ambazo zinamilikiwa na halmashauri zetu tutahakikisha zinakuwa na visima vya maji, ili kuweza kukabiliana na majanga haya ya moto,” aliandika Ummy.

Soko hilo liliungua katika upande wa juu huku wa chini (shimoni), kukiwa hakujaathirika na moto. Tangu tukio hilo kutokea Jeshi la Zima Moto na Uokoaji, linaendelea kuchukua jitihada za kuuzima.
Kwa sasa, Serikali imesitisha shughuli za soko hilo kwa muda wa siku saba, kuanzia jana Jumapili hadi tarehe Jumapili tarehe 18 Julai 2021, ili uchunguzi wa tukio hilo ufanyike.
Leo Jumatatu, Mwenyekiti wa Wafanyabiashara katika soko hilo, John Shayo, amesema wanatarajiwa kukutana mchana wa leo, kwa ajili ya kujadili namna ya kujikwamua katika tukio hilo.
“Leo mchana tunakutana ili tujue tunahitaji msaada wa aina gani, tutakapomaliza kikao tutajua hali ikoje na hatua za kuchukua,” amesema Shayo.
Shayo amesema wafanyabiashara wengi walioathirika na tukio hilo hawana bima za moto na kutoa wito kwa Serikali kupitia Shirika lake la Bima la Taifa (NIC), liwape elimu ili wakate bima hizo kwa ajili ya kuchukua tahadhari dhidi ya majanga.
Leave a comment