DURUya tatu ya mazungumzo kutoka kwa wajumbe wa nchi za Ukraine na Urusi, imepiga hatua na kusababisha Urusi kutangaza njia salama kwa raia wanaotaka kuondoka nchini humo. Anaripoti Mwandishi Wetu … (endelea)
Hatua hiyo imekuja baada ya duru ya kwanza na ya pili ya mazungumzo hayo yanayofanyika nchini jirani ya Belarusi kugonga mwamba.
Duru hiyo ya tatu ya mazungumzo yanayolenga kusitisha vita kati ya nchi Ukraine na Urusi ilimalizika jana jioni ya tarehe 7 Machi, 2022.
Mmoja wa maofisa wa Serikali wa Ukraine, amenukuliwa na Shirika la habari la Interfax akisema kumepatikana maendeleo madogo ambayo hakuyataja.
Hata hivyo, baada ya mazungumzo hayo, Urusi ilitangaza kuruhusu raia kuondoka kwenye miji ya Ukraine, ukiwemo mji mkuu, Kyiv, kuanzia saa 3:00 asubuhi ya leo tarehe 8 Machi, 2022.
Aidha, raia hao walitakiwa kutumia njia zinazopitia Urusi na Belarusi kuondoka nchini Ukraine jambo ambalo Ukraine imelikataa.
Imeelezwa kuwa raia wanaoondoka miji ya Kyiv, Chernigov na Kharkiv walitakiwa kuelekea Urusi kupitia Belarus.
Hata hivyo, watu wanaoondoka kwenye mji wa Sumy na Mariupol wamepewa fursa ya kuchagua ama kupitia Urusi au miji ya Ukraine ya Potlava na Zaporizhia.
Leave a comment