September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Morrison Pasua Kichwa, asimamishwa kwa muda Simba

Bernard Morrison akisaini mkataba wa kuitumikia Simba

Spread the love

 

UONGOZI wa klabu ya soka ya Simba umemsimamishwa kwa muda, kiungo mshambuliaji wake Bernad Morrison Raia wa Ghana kufuatia kuwa na matatizo ya utovu wa nidhamu aliouonesha kwenye kambi ya timu hiyo. Anaripoti  Mwandishi Wetu…(endelea)

Mchezaji huyo amesimamishwa kufuatia kuripotiwa kutoka kambini bila ruhusa kinyume na utaratibu uliowekwa na uongozi huo.

Taarifa ya ilitolewa hii leo tarehe 4 Februari 2022, na klabu ya Simba ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara ilieleza kuwa, mara baada ya Morrison kufanya hivyo, uongozi na benchi la ufundi ulimpa maelekezo ya kuwa asirejee kambini hapo mpaka atakapoonana na mtendaji Mkuu wa klabu hiyo, Barbara Gonzalenz.

Licha ya kupewa maelekezo hayo, mchezaji huyo hakuchukua hatua yoyote na hivyo kuendelea kukaa nje ya kambi ya timu hiyo, wakati kikosi hiko kikijiandaa na michezo mbalimbali ya Ligi Kuu na kombe la Shirikisho la Azam.

Sio mara ya kwanza kwa mchezaji huyo kuripotiwa kuwa na matatizo ya utovu wa nidhamu, ikumbukwe alipokuwa anakipiga ndani ya klabu ya Yanga, alishawahi kuondoka kambini nyakati za usiku na kutokomea kusiko julikana na kisha kuibukia upande wa pili wa klabu ya Simba.

Mara baada ya kusimamishwa kwa mchezaji huyo uongozi wa klabu ya Simba umemtaka Morrison atoe maelezo kwa njia ya maandishi kwa mtendaji mkuu wa timu hiyo, na kama akikaidi kufanya hivyo uongozi wa mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara umepanga kuchukua hatua kali.

Ikumbukwe mkataba wa mchezaji huyo kwa sasa unaelekea mwishoni, ukiwa umebakiza miezi sita toka aliposaini mwaka mmoja na nusu uliopita.

Morrison alisaini kuitumikia Simba katika kipindi cha miaka miwili kuanzia msimu wa 2020/21, mwezi Agosti.

error: Content is protected !!