KUELEKEA mtanange wa watani wa jadi, kiungo mshambuliaji wa klabu ya Simba, Bernard Morrison amechaguliwa kuwa mchezi bora wa mashabiki wa klabu hiyo, kwa mwezi Juni 2021. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).
Mchezaji huyo wa zamani wa klabu ya Yanga, ametwaa tuzo hiyo, ikiwa imesalia siku moja kabla ya mtanange wa watani wa jadi, utakaopigwa tarehe 3 Julai, 2021, kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, jijini Dar es Salaam.
Morrison ambaye ni raia wa Ghana, amewashinda nyota wawili wa klabu hiyo aliongia nao kwenye fainali ambao ni nahodha wa kikosi hiko John Bocco na Luis Miquisone.
Mchezaji huyo mwenye vituko vingi uwanjani, kwa mara ya kwanza atakuwa amevalia jezi ya Simba na kuvaana na klabu yake ya zamani ya Yanga kwenye mchezo huo wa watani wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Tuzo hiyo imeenda kwa Morrison baada ya kuibuka shujaa kwenye mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Azam FC, kwa kaunzisha mpira wa adhabu ndogo kwa haraka na kupelekea Luis Miquisone kupachika bao ambalo lilikuwa muhimu na la ushindi kwenye dakika za mwisho.
Mchezo huo dhidi ya Azam FC ulipigwa kwenye Uwanja wa Majimaji, Ruvuma mkoani Songea tarehe 26 Juni, 2021.
Morrison atakabidhiwa kitita cha Sh 1,000,000 kutoka kwa wadhamini Emirate Aluminium Profile ambao walianza kutoa tuzo hiyo tangu Februari mwaka huu.
Kwa mujibu wa klabu ya Simba, kura zilizopigwa ni 9,356 na Morrison alipata kura 6,697 sawa na asilimia 72, huku Miquisone akipata kura 1,978 sawa na asilimia 21, na Bocco alipata kura 681 sawa na asilimia saba.
Leave a comment