September 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Morogoro watenga 25% za mapato kutunza misitu

Spread the love

MADIWANI wa Halmashauri ya wilaya ya Morogoro wameazimia kutenga asilimia 25 wanayokusanya kutoka vijiji vya mradi wa mkaa endelevu kila mwaka na kuanzisha suala la usimamizi shirikishi wa misitu (USM) vijijini. Anaripoti Christina Haule, Morogoro … (endelea).

Madiwani hao walisema hayo wakati wakikamilisha kikao cha mrejesho wa shughuli za mradi wa kuleta mageuzi katika sekta ya mkaa Tanzania (TTCS) kilichofanyika mjini hapa. 

Walisema, Watalaamu wao wa misitu katika ngazi zote ni vema wakashirikiana katika mikutano ya vijiji huku Serikali za vijiji zikipewa mafunzo na kuelimishwa kutokuwa na utaratibu wa kubadilisha maeneo ya misitu kuwa mashamba bila utaratibu.

Aidha walisema Halmashauri ya Wilaya hiyo iweke bajeti ya kutengeneza mpango wa matumizi bora ya ardhi katika Wilaya na mpango huo uanze angalau kwa vijiji vitano kwa mwaka.

Pia walimtaka Mratibu wa mradi kupeleka mpango mkakati wa miaka mitano wa vijiji vinavyoingizwa kwenye matumizi bora ya ardhi na USM ikijumuisha misitu ya halmashauri ya wilaya na kuiwekea mipango ya usimamizi.

Hata hivyo walimtaka Mratibu wa Mradi wa TTCS wilayani humo ahakikishe taarifa zinafika kwenye vikao vyao vya robo mwaka hususan taarifa zinazohusu uendelevu wa matumizi wa maliasili kwenye vijiji vya mradi na vijiji vingine ili viwe na mwenendo mzima wa vijiji kama sheria na kanuni zinavyotaka.

Hivyo walimtaka Mratibu wa Mradi wa TTCS Mwanasheria na wataalamu wa MJUMITA wamalizie rasimu kwa kupitia kwenye vijiji husika ili wapate maoni na wawakilishe taarifa hizo katika vikao vya robo vya mwaka zinapatikana.

Warsha hiyo ilihudhuriwa na wajumbe 66 wakiwemo Baraza lote la Waheshimiwa Madiwani wa Halmashauri ya Wilaya ya Morogoro, Wakuu wa Idara mbalimbali zikiwemo Idara ya Maliasili na Ardhi, Idara ya Kilimo, Idara ya Maendeleo ya Jamii, Idara ya Mazingira na Afisa Maliasili (W).

error: Content is protected !!