August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mongella ‘ajiongeza’ uchangiaji madawati

Spread the love

JOHN Mongella, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza amejiongezea muda wa kutekeleza agizo la Rais John Magufuli la kuhakikisha uhaba wa madawati katika shule za umma linakoma, anaandika Moses Mseti.

Machi 15 mwaka huu, Rais Magufuli wakati akiapisha wakuu wa mikoa Ikulu jijini Dar es Salaam, aliwataka kuhakikisha wanatatua tatizo la madawati kwa shule za umma ifikapo Juni 30 mwaka huu jambo ambalo kwa Mkoa wa Mwanza halijakamilika.

Kutokana na hali hiyo, Mongella amejiongezea muda huo kwa madai kutokana na uhaba wa rasilimali fedha na kwamba, zoezi hilo litakamilika mwishoni mwa Agosti Mwaka huu.

Mongella akizungumza na waandishi wa habari jana amesema, mpaka sasa mkoa wake una upungufu wa madawati kiasi cha 5,931 kwa shule za sekondari ni sawa na asilimia 5.25 na kwa shule za msingi upungufu ni madawati 52, 456 sawa na asilimia 22.26.

Mongella amesema kuwa, katika mkoa huo wenye shule za sekondari 197 na wanafunzi 110,024, una mahitaji ya madawati 112,997, awali yalikuwe madawati 101,741 huku yaliotengenezwa hivi sasa kuwa ni 5,325 na kufikisha idadi ya madawati 107, 066 sawa na 94.75.

“Tunaendelea na zoezi la kutengeneza madawati licha ya kwamba zoezi hili lilitakiwa likamilishwe Juni 30 mwaka huu, zoezi hili litakamilishwa mpaka kufikia Agosti 30 mwaka huu, tutakuwa tumemaliza kutengeneza,” amesema Mongella.

Mongella amesema kuwa, tatizo kubwa la madawati lipo katika Shule za Msingi, ambapo kwa Mkoa wa Mwanza una jumla ya shule 851, wanafunzi 640, 695 na mahitaji kamili ya madawati ni 237, 968.

Hata hivyo, madawati yaliokuwepo kabla ya agizo la rais yalikuwa 115, 540 na kwa sasa madawati mapya yaliotengenezwa ni 69, 972 sawa na asilimia 77. 74.

Amesema kuwa, sababu kubwa kwa zoezi hilo kuchelewa kutekelezeka kwa wakati ni uchache wa rasilimali fedha na kwamba, wamefanikiwa kutengeneza madawati kwa kiasi kikubwa.

“Kiasi cha fedha Sh. Milioni 68 ambacho kilipangwa awali kutumika katika michezo ya Umitashumta na Umiseta, chote hivi sasa kimeelekezwa katika kutengeneza madawati, pia vikao katika mkoa huu vimefutwa vyote,” amesema Mongella.

error: Content is protected !!