December 5, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mongela: Hakuna baba anayetaka mwanamke anayenuka moshi, tukomboke!

Balozi Getrude Mongella

Spread the love

 

MWANASIASA mkongwe na mwanaharakati wa masuala ya wanawake, Balozi Getrude Mongella ametoa wito kwa wanawake kujikomboa kutoka kwenye matumizi ya nishati chafu ya kupikia na kuhamia kwenye nishati safi kwa kuwa hakuna mwanaume anayemtaka mwanamke anayenuka vumbi au moshi wa kuni na mkaa.

Amesema hana wasiwasi na wanaume kuunga mkono ajenda ya matumizi ya nishati safi na ya kupikia kwani wao pia wanataka wanawake wakomboke na kurudi kwenye maisha ambayo yataimarisha uchumi wao na Taifa kwa ujumla. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Mongela ametoa wito huo jijini Dar es Salaam jana tarehe 2 Novemba, 2022 wakati akichangia mada katika kongamano la Mjadala wa Kitaifa wa Nishati safi ya Kupikia lililoandaliwa na Wizara ya Nishati.

Mongela ambaye alikuwa akichangia mada kuhusu ‘Mchango wa Wanawake katika kuhakikisha matumizi ya nishati safi inapigiwa chapuo’, alisema kwa kuwa Tanzania ilikabiliana na matatizo mengi na kufanikiwa kuvuka, pia kwenye kuachana na nishati chafu itafanikiwa kuvuka.

“Akina baba hawana tatizo katika kuunga mkono hili kwa sababu hakuna baba anayetaka mwanamke aje kitandani akiwa ananuka moshi, vumbi.. Na wao akina baba wanataka wanawake tukomboke…turudi katika maisha ambayo yataimarisha uchumi wa Taifa letu,” alisema.

Alisema kwa kuwa Rais Samia Suluhu Hassan amewaagiza viongozi kuwa wawaondoe wanawake katika madhara wanayopata kwa kutumia nishati chafu, hakuna yeyote anayepaswa kukataa kutekeleza maagizo hayo.

Aidha amesema katika uchaguzi ujao mbunge atapata kura kulingana na idadi ya mitungi ya gesi aliyowagawia wananchi wake badala ya khanga na vikombe vya kunywea gongo.

“Akina mama wabunge tumepewa homework kwenda kufanyia kazi na kwa wanaume kura zenu zitahesabiwa kulinga na mitungi mingapi mmesambaza kwenye majimbo.

“Hiyo ni ajenda kwetu sisi wasema hovyo tunaenda mitaani kuhakikisha kura za mtu zinahesabika kulingana na mitungi sio kusubiri wakati wa uchaguzi kutugawia vikanga na vikombe vya gongo hapana!… tunataka mitungi ya gesi,” amesema.

Hata hivyo, amemtaka Waziri wa Nishati, Januari Makamba asiwe na wasiwasi katika kutekeleza ajenda hiyo ya nishati safi kwa kuwa ngoma imepata wachezaji.

“Tunataka turudi katika mazingira ya matumizi ya nishati safi ambayo yanaendana na sisi wanawake tulioumbwa na Mwenyezi Mungu kwa kutumia nyama na sio udongo kama wanaume… kwa hiyo nishati chafu inatupunguzia hadhi yetu, inatunyima muda wa kupumzika, kutumia vipaji vyetu,” alisema.

Alisema akina mama ni sehemu tu ya watu wanaopaswa kushiriki kusukuma ajenda ya nishati safi kwa sababu hawakupewa jukumu la kupika bali ni jamii ndio imewatutwisha mzigo huo wa kupika.

error: Content is protected !!