August 13, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Kutoka Bungeni leo

Spread the love

GEORGE Simbachawene, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(Tamisemi) amesema, tabia ya wakuu wa mikoa na wilaya kuomba mafuta kwa wakurugenzi hairuhusiwi kwa kuwa, ni kinyume na taratibu, anaandika Dany Tibason.

Hata hivyo, amesema viongozi wanaofanya hivyo wanapaswa kufahamu  kuwa, wanavunja sheria na wizara  italichunguza jambo hilo na kuwawajibisha wahusika watakaobainika kufanya hivyo.

Simbachawene ametoa kauli hiyo leo bungeni wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Chemba, Juma Nkamia (CCM).

Mbunge huyo  aliyetaka kujua serikali ina mpango gani wa kuboresha maslahi ya wakuu wa mikoa na wilaya ili kuwapunguzia hali ya kuwa ombaomba kwa wakurugenzi wa halmashauri na majiji.

“Wakuu wa mikoa wanaishi kwa fadhila za wakurugenzi na kwa mara kadhaa wamekuwa wakisikika  wakiomba mafuta, je, serikali haioni umuhimu wa kuwaongezea  maslahi,” amehoji Nkamia.

Waziri huyo amekiri kuwepo na taarifa za wakuu wa mikoa na wa wilaya wanaoomba mafuta kwa wakurugenzi  na kwamba, haikubaliki.

Amesema, kwa kuwa si katika maeneo yote matukio hayo yameripotiwa lakini kama wanaofanya  hivyo wanaenda kinyume na sheria.

Jimbo la Mtera

Ahadi za rais wa awamu ya nne zimeendelea kuwatesa wabunge wengi kutokana na ahadi hizo kushindwa kutekelezwa ndani ya muda muafaka.

Leo bungeni, Livingston Lusinde, Mbunge wa Mtera ametaka kujua ahadi za rais wa awamu ya nne (Rais Mstaafu, Jakaya Kikwete) za ujenzi wa barabara zitakamilika lini.

Katika swali lake la msingi la Lusinde amehoji, ni lini ujenzi wa barabara hiyo utaanza kujengwa kwa kiwango cha lami kama ilivyoahidi wana Rais Kikwete na rais wa awamu ya tano (Dk. John Mgufuli) ambaye alisisitiza kwamba, barabara hiyo itajengwa haraka.

Akijibu swali hilo Edwin Ngonyani, Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano amesema, serikali inayo azma ya kujenga kwa kiwango cha lami barabara ya Mlowa Barabarani -Mvumi Misheni kwenye Hospitali Teule ya Wilaya ya Chamwino.

Ngonyani ametoa kauli hiyo leo bungeni wakati akijibu swali la  Mbunge wa Mtera, Livingstone Lusinde (CCM).

Akijibu swali hilo, Naibu Waziri huyo amesema, ni kweli Rais Kikwete alitoa ahadi hiyo na pia Rais Magufuli na kwamba, itajengwa kulingana na upatikanaji wa fedha.

“Serikali inatambua umuhimu wa barabara hii kwa jamii na hususan katika kusaidia wagonjwa wanaoenda kupata huduma ya matibabu katika Hospitali ya Mvumi Mission.

“Azma ya kujenga barabara hii ipo pale pale na itatekelezwa kulingana na upatikanaji wa fedha,”amesema Ngonyani.

Aidha amesema, kwa sasa barabara hiyo itaendelea kuhudumiwa na serikali kupitia Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) kwa kufanya matengenezo ya aina mbalimbali kwa kiwango cha changarawe kwa kutumia fedha za Mfuko wa Barabara ili iendelee kupitika majira yote ya mwaka.

Jimbo la Nkasi Kusini

SERIKALI imesema kwamba, kupitia Mamlaka ya Mapato nchin (TRA), imeanza mchakato wa kuboresha sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1973 kutokana na wananchi kulalamikia sheria hiyo kwa muda mrefu.

Hayo yamebainishwa leo bungeni na Dk. Ashatu Kijaji, Naibu Waziri wa Fedha na Mipango alipojibu swali la Mbunge wa Nkasi Kusini, Desderius Mipata (CCM).

Katika swali la msingi Mipata aliihoji serikali na kuitaka ieleze kama haioni umuhimu wa kuitazama upya sheria hiyo ambayo husababisha kudaiwa kodi hata kipindi ambacho gari halifanyi kazi.

“Kwa kuendelea kutumia sheria hiyo  serikali haioni kwa kufanya hivyo inakuwa inawaibia wananchi wake,”amehoji Mipata na kuongeza;

“Kodi hii imekuwa ikilalamikiwa sana na wananchi kwa kuwa, imekuwa ikidaiwa hata magari mabovu au ambayo yamepaki kwa muda wote bila kujali kipindi ambacho gari ilikaa bila kufanya kazi.

Akijibu swali hilo, Dk.Kijaji amesema, kodi ya magari inasimamiwa chini ya sheria ya usalama barabarani ya mwaka 1973 pamoja na kanuni zake ambapo imekuwa ikifanyiwa marekebisho mara kwa mara kulingana na mahitaji ya wakati husika.

Amesema, kodi hiyo ni moja ya kodi zinazokusanywa na TRA na kwa mujibu wa kanuni za usalama barabarani na ushuru wa magari sura ya pili, kifungu cha 4 na 5, hakuna msamaha wa leseni ya gari kwa mtu yeyote.

Amesema, sheria inataka ada hiyo kulipwa kila mwaka tangu gari husika liliposajiliwa na hivyo sheria haitoi unafuu wowote kwa gari lililosimama kwa muda mrefu bila kutembea barabarani.

“Ni kweli, utekelezaji wa sheria hii unaleta adha kwa wamiliki wa magari na hasa pale ambapo kuna ushahidi wa kutosha kwamba, gari husika limesimama kwa muda mrefu kwa sababu za msingi,” amesema Dk. Kijaji.

Aidha amesema, ili kuondoa adha hiyo, mamlaka hiyo imeanza mchakato wa kuboresha sheria hiyo ikiwa ni pamoja na kutoa mapendekezo ya namna bora ya kuhudumia wamiliki wa magari ambayo yamesimama kwa kipindi kirefu bila kutembea barabarani kwasababu za msingi.

Amebainisha baada ya taratibu zote kukamilika, mapendekezo ya mabadiliko ya sheria hiyo yatapelekwa bungeni ili kujadiliwa na kuidhinishwa na Bunge kwa kadri itakavyoonekana inafaa.

Jimbo la Nkasi Kaskazini

SERIKALI inatarajia kupeleka kiasi cha Sh. Milioni 550 katika Jimbo la Nkasi Kaskazini kwa ajili ya kukamilisha mradi wa kilimo cha umwagiliaji katika bonde la mto Lwafi.

Kauli hiyo ilitolewa jana Bungeni na Naibu Waziri wa Maji na Umwagiliaji,  Isack Kamwelwe wakati akijibu swali la nyongeza la Mbunge wa Nkasi Kaskazini , Ally Keissy (CCM)

Katika swali la nyongeza mbunge huyo alitaka kujua ni kiasi gani cha fedha kitatolewa na serikali kukamilisha Mradi huo ambao unaonekana kusuasua kwa muda mrefu.

Awali katika swali la msingi Kessy alitaka kujua ni lini Serikali itapeleka fedha ili kukamilisha mradi wa Skimu Lwafi ili kukamilisha mradi huo ili uwe msaada kwa wakulima wa mpunga zaidi ya 4,000 huku akisema mradi huo  tayari umeshatumia sh. Milioni 800 na hakujawanufaisha wakulima hao.

Akijibu swali hilo, Kamwelwe alisema serikali itapeleka fedha hizo mwezi juni, mwaka huu ambazo zimetokana na mkopo kutoka serikali ya Japan.

Kamwelwe alisema Serikali kwa kuzingatia mahitaji ya wananchi wa tarafa ya Kilando kuhusu uendelezaji wa kilimo hicho na kuboresha miundombinu ya umwagiliaji katika skimu husika kwa awamu kulingana na upatikanaji wa fedha.

Hata hivyo alisema Mnamo mwaka 2012 banio lilijengwa na mfereji mkuu wa urefu wa kilomita 1.6 ulichimbwa na kusakafiwa.

Naibu huyo alisema fedha hizo zitatumika kuchimba sehemu ya mfereji mkuu wenye urefu wa kilomita 16 na kuusakafia na kujenga maumbo ya maji ndani ya mfereji huo na hatua hiyo itawezesha wakulima wa mpunga katika skimu hiyo kunufaika.

 

error: Content is protected !!