August 9, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Moitoi: Afrika inaogopa nini ICC?

Spread the love

PELONOMI Venson Moitoi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Botswana na mgombea wa nafasi ya Mwenyekiti wa Tume ya Afrika (AUC), amepinga uamuzi wa baadhi ya nchi za Afrika kujitoa katika Mahakama ya Makosa ya jinai (ICC), anaandika Wofram Mwalongo.

Moitoi amejitosa kupinga hoja za nchi mbalimbali za Afrika zinazojitoa ICC na kusema hakuna ulazima wa kujitoa kwani kuna nafasi ya kupeleka malalamiko yao na yakafanyiwa kazi.

Amesema ni vyema waafrika wakashirikiana kuishinikiza Mahakama ya Afrika kushirikiana na (ICC).

“Sioni kwanini tujitoe, kitu kizuri ni kuwa wanachama wachache wa ICC, wanakubaliana kimsingi kuwa hakuna haja ya nchi za Afrika kujiondoa kwa sababu sio suluhu ya tatizo. Tunapaswa kufanya kazi pamoja kutatua tatizo sio kuongeza tatizo”. Amesema Venson-Moitoi.

Moitoi ameshikilia mtazamo wake huo ambao huenda ukawa sababu ya yeye kukwama kukalia kiti hicho, ingawa anasimamia demokrasia na utawala bora ambapo mwaka huu, nchi yake ni miongoni mwa nchi tatu zilizoshinda tuzo ya utawala bora katika nchi za Afrika zikiwemo pia Mauritius na Cape Vede.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema, mtazamo wa kiongozi huyo huenda ikawa tiketi ya kumpa ushindi Amina Mohamed, Waziri wa Mambo ya Nje wa Kenya anyeunga mkono mataifa ya Afrika kujitoa katika Mahakama hiyo.

Uchaguzi wa kumpata mrithi wa Nkosazana Dlamini-Zuma aliyekuwa mwenyekiti wa Tume hiyo Kutoka Afrika kusini unatarajiwa kufanyika mwezi januari mwakani. Ambapo mpaka sasa mataifa ya Kenya, Burundi, Afrika kusini na Gambia yameweka wazi kwamba hawataki kushirikiana na Mahakama hiyo.

error: Content is protected !!