August 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

MOI wakana kufyeka kiholela miguu majeruhi bodaboda

Hospitali ya Muhimbili kitengo cha Mifupa (MOI)

Spread the love

MKURUGENZI wa Taasisi ya Tiba ya Mifupa Muhimbili (MOI), Dk. Respicious Boniface amesema si kweli kwamba majeruhi wa ajali za bodaboda hukatwa miguu kila wanapofikishwa katika taasisi hiyo bila kufanyiwa uchunguzi wa kina. Anaripoti Danson Kaijage, Dodoma … (endelea).

Mkurugenzi huyo ametoa kauli hiyo kutokana na uvumi ulioenea katika mitandao ya kijamii kwamba majeruhi wa ajali za pikipiki wanaofikishwa katika taasisi hiyo kupatiwa matibabu hukatwa miguu hata kama majeraha yao hayastahili kupatiwa tiba ya aina hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari leo tarehe 28 Julai, 2022 kuhusu utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Taasisi hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja, Mkurugenzi huyo amesema mafunzo yao hayawaongozi kutoa tiba ya aina hiyo.

“Sisi mafunzo yetu yanatutaka kwanza kuangalia namna ya kuokoa kiungo badala ya kukikata hata kama mfupa umevunjika vunjika mara nyingi, tunatakiwa kutoa uangalizi wa masaa 12 baada ya hapo kama utakuwa unaweza kuleta madhara katika jeraha lile ndipo tunapaswa kuukata” amesisitiza Dk. Boniface

Aidha, Dk. Boniface amesema majeruhi wengi wanaopatiwa matibabu katika taasisi hiyo ni wa ajali za pikipiki (bodaboda) pamoja na magari.

Kutokana na hali hiyo amewataka Watanzania kuzingatia sheria za usalama barabarani ili kuipunguzi mzigo serikali wa kuhudumia majeruhi hao.

Aidha, amesema serikali imetoa Sh. bilioni 4.2 kwa ajili ya ununuzi wa upandikizaji wa tishu (implants) ili kukabiliana na changamoto hiyo kwa wagonjwa.

“Vifaa hivi vimesaidia kuendelea kuboresha huduma za matibabu ya kibingwa ya mifupa, ubongo, uti wa mgongo na mishipa ya fahamu, hivyo kuokoa maisha ya Watanzania wengi na pesa za serikali ambazo zingetumika kupeleka wagonjwa nje ya nchi kwa matibabu,” ameeleza Dk. Boniface

Pia, amesema kwamba katika kipindi cha mwaka mmoja jumla ya wagonjwa 7,113 walifanyiwa upasuaji ikilinganishwa na wagonjwa 6,793 waliofanyiwa katika mwaka uliopita wa 2020/2021 ikiwa ni ongezeko la asilimia 2.

“Upasuaji mbalimbali wa kibingwa uliofanyika ni pamoja na kubadilisha nyonga 207 kubadilisha magoti 182 upasuaji wa mfupa wa kiuno 96, Wagonjwa 200 wamefanyiwa upasuaji wa magoti na mabega kwa njia ya matundu kati yao waliofanyiwa mabega ni 32 na magoti ni 168, wagonjwa 249 wamefanyiwa upasuaji wa uti wa mgongo kwa kufungua eneo dogo,” ameeleza.

Ameongeza kuwa katika kipindi hicho cha mwaka mmoja watoto 17 wamefanyiwa upasuaji wa kunyoosha vibiongo wagonjwa 11wamefanyiwa upasuaji wa kuondoa vivimbe vya mishipa ya damu kwenye ubongo.

“Gharama za matibabu haya ndani ya nchi zilikua Sh. bilioni 10.2 na kama wangepelekwa nje ya nchi kwa matibabu jumla ya Sh. bilioni 42.7 zingetumika. Hivyo taasisi imeokoa Sh. bilioni 32.5, ambazo zitatumika kwa shughuli nyingine za maendeleo ya nchi,” amesema.

Amesisitiza kuwa huduma mpya zilizoanzishwa na Taassi hiyo katika kipindi hicho kuwa ni huduma ya kuondoa uvimbe kwenye sakafu ya ubongo kupitia tundu la pua ambapo Wagonjwa 19 wameshafanyiwa upasuaji.

“Gharama za upasuaji huu hapa nchini ni Sh. milioni 8 na nje ya nchi ni Sh. milioni 40 hivyo Taasisi imeokoa zaidi ya Sh. milioni 608,000,000 ambazo zingetumika kupeleka wagonjwa hawa nje ya nchi,” amesema.

Aidha, ameeleza kuwa huduma nyingine ni matumizi ya maabara ya upasuaji wa Ubongo ambapo katika kipindi hiki wagonjwa 186 wamehudumiwa.

Amesema gharama za huduma hiyo nchini ni kati ya Sh. milioni tano hadi 10 na nje ya nchi ni Sh. million 30 hadi 60 hivyo Taasisi imeokoa kati ya Sh. bilioni 5.6 hadi Sh. bilioni 11.2 ambazo zingetumika kupeleka wagonjwa hawa nje ya nchi.

“Huduma hizi mpya, zimeiwezesha taasisi kupunguza kwa kiasi kikubwa rufaa za wagonjwa nje ya nchi. Ambapo kwa sasa kwa magonjwa ya Neurosurgeries 96% tunafanya hapa na Upasuaji wa mifupa 98% tunafanya hapa,” ameeleza.

error: Content is protected !!