Monday , 11 December 2023
Home Kitengo Habari Kimataifa Mohammed Deif: Paka mwenye roho tisa anayeongoza kundi Hamas
KimataifaMakala & Uchambuzi

Mohammed Deif: Paka mwenye roho tisa anayeongoza kundi Hamas

Spread the love

WAKATI vita kati ya Israel na Palestina ikizidi kushika kasi na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 2000, asilimia kubwa ya wafuatiliaji wa vita hiyo wamekuwa wakijiuliza ni nani aliyenyuma ya Hamas – kundi la Kiislamu la Palestina ambalo linaendesha shughuli zake katika ukanda wa Gaza.

Huyu si mwingine bali ni Mohammed Deif ambaye ni kamanda wa Jeshi hilo la Hamas aliyetoa wito kwa Wapalestina siku ya Jumamosi tarehe 7 Oktoba, 2023 kwamba kila mmoja ajiunge na operesheni ya kundi hilo. Muda mchache baadae wapiganaji wa kundi lake walivamia Israel na kusababisha maafa mabaya.

“Tumeamua kukomesha makosa haya ya Israel kwa msaada wa Mungu, hivyo adui anaelewa kuwa muda wa kufanya uharibifu bila kuwajibishwa umekwisha,” alisikika Kamanda huyo anayetajwa kuwa na roho saba kama mnyama paka.

MOHAMMED DEIF NI NANI?

Rekodi ya sauti inayokwaruza ya mwanamgambo wa Palestina ilituma onyo la kutisha kwa Israeli mwaka 2021.

Sauti hiyo iliyorekodiwa inasema Israeli italipa ikiwa haitatimiza matakwa ya Hamas, kundi la Kiislamu la Palestina ambalo linaendesha shughuli zake katika ukanda wa Gaza.

Sauti hiyo ilikuwa ya Mohammed Deif, mmoja kati ya wanaume wanaotafutwa kwa udi na uvumba na Israeli. Deif alikuwa amevunja ukimya wake kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka saba.

Lakini baada ya ujumbe wake kupuuzwa, vita vilitokea na kutikisa Israeli na Gaza kwa zaidi ya siku 11 kabla ya kufikiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano.

Takriban watu 242 waliuawa huko Gaza, kulingana na Umoja wa Mataifa huku wengine 13 wakiuawa huko Israeli wakati wa vita hivyo vilivyotokea kati ya Mei 10 na 21 mwaka 2021.

Umoja wa Mataifa unasema watu 129 kati ya waliouwa huko Gaza walikuwa raia. Wanajeshi 200 wa Israel waliuawa wakiwamo wanamgambo 80 wa Hamas. Pia alikuwemo kiongozi wa kundi la Hamas, Yahya Sinwar. Ingawa Deif hakuwa miongoni mwa waliouawa.

“Wakati operesheni hiyo inatekelezwa, tulikuwa tumejaribu kumuua Mohammed Deif,” Msemaji wa kikosi cha ulinzi cha Israel Hidai Zilberman anasema kwa mujibu wa gazeti la New York Times.

Majaribio mawili ya kumuua Deif yalifanyika wakati wa mapigano hayo, afisa wa kikosi cha jeshi cha Israeli amethibitishia BBC. Kushindwa kumuua kulimwezesha kunusurika kifo angalau mara saba katika kipindi cha miongo miwili.

Mchezo huu wa paka na panya umeumiza kichwa jeshi la Israeli ambalo lililenga kusababisha mauaji dhidi ya makomanda wengi wa Hamas wakati wa vita vya hivi karibuni.

“Walikuwa na orodha ya watu wanaoamini walikuwa na uwezo mkubwa wa kijeshi katika kundi la Hamas na aliyekuwa analengwa wa kwanza kabisa alikuwa Mohammed Deif,” mchambuzi wa masuala ya Mashariki ya Kati, Matthew Levitt amezungumza na BBC.

Mengi yanayoyafahamika kuhusu Deif yanatoka katika vyombo vya habari vya Israeli na Palestina.

Inaelezwa kuwa Deif alizaliwa mji wa Gaza katika kambi ya Khan Yunis mwaka 1965, wakati eneo hilo lilikuwa limekaliwa na Misri.

Jina lake ni Mohammed Diab Ibrahim al-Masri lakini kupitia maisha yake ya kuhama hama kukwepa mashambulizi ya anga ya Israeli, baadaye alianza kufahamika kama Deif jina linalomaanisha “mgeni” kwa lugha ya Kiarabu.

Ni machache sana yanayofahamika kuhusu alivyokuzwa katikati ya mgogoro kati ya Israeli na Palestina ambao athari zake haziwezi kusahaulika katika eneo la Mashariki ya Kati.

Deif alikuwa kijana mdogo wakati kundi Hamas linaundwa, akijiunga nalo miaka ya 1980.

Akiwa amejitolea kupigana dhidi ya Israeli, mara moja Deif alianza kupata umaarufu ndani ya kikosi cha Hamas cha Izzedine al-Qassam.

“Anachukuliwa kuwa afisa wa Hamas mwenye msimamo mkali,” amesema Levitt aliyekuwa mshauri wa masuala ya kukabiliana na ugaidi katika Wizara ya Marekani.

Levitt ameongeza kuwa Deif alikuwa karibu na baadhi ya makamanda wa Hamas, kama vile Yehya Ayyash, mtengenezaji mabomu maarufu aliyekuwa akijulikana kama injinia.

Ayyash alilaumiwa kuhusiana na baadhi ya mashambulizi mabaya ya mabomu huko Israeli mapema miaka ya 1990. Baada ya kuuawa na Israeli mwaka 1996, mashambulizi zaidi ya mabomu yakafuata.

Mwanafunzi wa Ayyash, Deif alishutumiwa kwa kutekeleza mashambulizi hayo kama njia ya moja ya kulipiza kisasi pamoja na wengine kuelekea upande wa Israeli.

Hatua hiyo iliongeza umaarufu wa Deif pamoja na cheo chake. Mwaka 2002, akapandishwa ngazi na kuwa kiongozi wa jeshi la Hamas kufuatia mauaji ya mwanzilishi wa kundi hilo, Salah Shehadeh.

Kama kiongozi, Deif amekuwa akipewa majukumu ya kuunda silaha za kundi la Hamas, roketi za Qassam, na usimamizi wa mahandaki huko Gaza.

Inasemekana kuwa wakati wa mapigano, Deif alikuwa amejificha ndani ya mahandaki hayo na kukwepa uvamizi wa jeshi la Israeli huku akiwa msimamizi wa operesheni ya kundi la Hamas.

PAKA MWENYE ROHO TISA

Kwa Deif, kuendeleza uwepo wake kumekuwa suala la ama kifo au kuendelea kuishi.

Miaka ya 2000 alinusurika mauaji ya Israeli ambako inasemekana alijeruhiwa vibaya, majeraha aliyopata ikiwa ni pamoja na kupoteza uwezo wake wa kuona katika jicho moja na kuvunjika miguu.

Aliyekuwa jasusi wa Israeli alithibitisha kwamba Deif alipata majeraha mabaya baada ya shambulizi la anga la Israeli dhidi ya nyumba yake mwaka 2006.

“Watu walifikiria kuwa hataweza kuendelea na majukumu yake tena kama mratibu wa jeshi,” jenerali mmoja wa Israeli aliyestaafu alizungumza na BBC.

“Lakini alifanikiwa kupata ahueni na kupona, licha ya kupoteza uwezo wa kuona wa jicho moja.”

Majaribio ya kumuua dhidi yake hayakufanikiwa na hatua hiyo ilimpatia jina la “paka mwenye roho tisa” miongoni mwa maadui zake.

Jaribio la tano la kumuua Deif lilifanyika katika operesheni ya 2014 iliyofanywa na Israeli katika ukanda wa Gaza.

Israeli ilianzisha mashambulizi ya anga katika eneo la Sheikh Radwan jirani na Gaza, na kusababisha mauaji ya mke wa Deif, Widad, na kijana wao mdogo, Ali. Wakati huo, Israeli ilifikiria kwamba pia Deif ameuawa lakini kumbe hakuwa nyumbani.

Muda mfupi baada ya hapo, kundi la Hamas likasema kuwa Deif bado “yupo hai na anaongoza operesheni” dhidi ya Israeli.

Deif inaaminika kwamba bado ndiyo msimamizi wa kundi hilo.

Juhudi za Israeli kumtafuta Deif zinaendelea. Licha ya umaarufu wake bado ni mtu asiyefahamika na wengi.

Katika mitaa ya Gaza, watu kidogo tu ndio ambao wanaweza kumtambua Deif ingawa wanamzungumzia vizuri kwa majukumu yake anayotekeleza.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

Kimataifa

Sakata la uhamiaji Rwanda lamng’oa waziri Uingereza

Spread the loveWaziri wa Uhamiaji wa Uingereza, Robert Jenrick amejiuzulu baada ya...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Uongozi wa Samia kuendelea hadi 2030

Spread the loveKWETU sisi tuliowahi kusoma sekondari, iwe O levo au A...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Bado askari wastaafu wanaonewa

Spread the loveRAIS wangu Samia Suluhu Hassan tunaendelea kumshukuru Mungu kwamba wote...

Habari za SiasaMakala & Uchambuzi

Tunastawisha ufisadi na kuchukia matunda yake

Spread the loveBUNGE la Jamhuri linaloendelea mjini Dodoma, kwa wiki nzima limetawaliwa...

error: Content is protected !!