June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

MOAT wajipanga kuzui muswada wa habari

Mwenyekiti wa Umoja wa Wamiliki wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), Dk. Reginald Mengi (kushoto), akizungumza (hawapo pichani) kuhusu muswada wa sheria ya vyombo vya habari. Kulia ni Mwanasheria, Godfrey Mpandikizi.

Spread the love

WAMILIKI wa Vyombo vya Habari Tanzania (MOAT), wameupinga Muswada wa Sheria ya vyombo vya habari unatarajiwa kusomwa bungeni mara ya pili katika mkutano wa Bajeti unaoendelea. Anaandika Sarafina Lidwino … (endelea).

Kikao cha MOAT kilichokutana leo jijini Dar es Salaam, kilimwalika mwanasheria wa Haki za Binadamu, Godfrey Mpandikizi ili kuvichambua vipengele vinavyofinya uhuru wa vyombo vya habari katika muswada huo.

Mpandikizi amebainisha matatizo na kero zilizopo katika muswada huo kuwa ni; adhabu za kutisha katika vifungu vya (36-41), kwamba kinamtia uoga mwandishi katika kufanya kazi.

Kipegele kingine ni kifungu cha (18b) kinachohusu kusajiliwa kwa waandishi wa habari na kufutwa na bodi husika, ambapo amesema kifungu hicho ni hatari kwa waandishi.

Amesema utoaji na ufutaji leseni kifungu cha (6d) na (6e), utatoa mwanya kwa Serikali kukifuta chombo cha habari bila kupita mahakamani.

Amefafanua kuwa, kifungu cha 14b(iv), ambacho kinalazimisha vyombo binafsi vya habari kujiunga na vyombo vya utangazaji vya Serikali ifikapo saa mbili kwa ajili ya taarifa ya habari, jambo hilo sio zuri na litakuwa na athari kubwa kwa wamiliki.

Mpandikizi ametaja pia kifungu cha 13(2), kinachosema, “hakuna mtu atakaye ruhusiwa kumiliki sehemu kubwa ya vyombo vya habari nchini”, akidai jambo hilo limeibua utata mkubwa na kuonekana kuwabana wawekezaji.

“Pia, kifungu cha 39(4) kinamruhusu afisa wa polisi kukamata mtambo wa uchapishaji iwapo inahisiwa kuandika habari za uchochezi. Kifungu hiki pia kinawanyima haki za msingi wamiliki na kuwapa polisi mamlaka mabaya,” amesema.

Mwanasheria huyo, amefafanua kuwa sheria ya kusimamia maadili ya kitaaluma,  serikali imejipa jukumu ambalo haliwahusu na kwa kwamba, hilo ni jukumu la Bodi. 

Pia, kifungu cha 42, kisemacho “endepo mtendaji au wakala atafanya makosa katika uandishi basi mmiliki pia atawajibika”, hiyo ni kuonesha jinsi serikali ilivyo ya ajabu.

“Sheria hii itatumika Tanzania Bara tu na sio Zanzibar wakati vyombo vya habari vipo kote,”amesema.

Katika majadiliano hayo, wajumbe mbalimbali wa MOAT walitoa michango yao, ambapo mmiliki wa makampuni ya IPP Media, Regnald Mengi, amekubaliana na wajumbe wengine kuupinga muswada huo.

Amesema, “Muswada huu ni wa kipumbavu, haufai kabisa kujadiliwa bungeni, wanapoteza tu muda wa kufanya mambo ya muhimu”.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya HaliHALISI Publishers Ltd (HHPL), Saed Kubenea, amesema muswada huo ukifika bungeni utavunja Katiba ya nchi.

“Kwa ufupi, sheria hii ni chafu haikubaliki, labda cha kuishauri Serikali isitishe mjadala huu. Tunamsubiri Rais ajaye ndipo tutajadili. Wameshatung’oa meno, macho na kuua kabisa sasa hivi wanatupeleka mahakamani,”amedai Kubenea.

MOAT  wameafikiana kuunda kamati ya kwenda bungeni kuzuia mapendekezo hayo yasijadiliwe kabla ya kushirikiana na wadau wengine wakiwemo wabunge wenye nia nzuri na vyombo vya habari.

error: Content is protected !!