January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mnyika: Kikwete amewaacha wananchi njiapanda

Rais Jakaya Kikwete akiwa na mmoja ya mwananchi mwenye ulemavu

Spread the love

MBUNGE wa Ubongo, John Mnyika, amemtaka Rais Jakaya Kikwete, kulieleza taifa kwa nini ameshidwa kutekeleza ahadi yake aliyoitoa wakati akizundua Bunge la Jamhuri, Novemba 2005. Anaandika Pendo Omary …. (endelea).

Kile ambacho Mnyika amekiita kimeshindwa kutekelezwa na Rais Kikwete, ni ahadi kuwa anatambua “maji ni kero nambari wani” na kwamba serikali yake itaandaa mpango kabambe wa kuhakikisha “tatizo la maji linakuwa historia nchini.”

Mnyika alitoa kauli hiyo jijini jijini Dar es Salaam, wakati akizungumza na waandishi wa habari.

“Rais Kikwete ameonesha udhaifu mkubwa wa kutekeleza ahadi zake alizozitoa kwa wananchi. Mwaka 2010 alilieleza Bunge kuwa serikali yake itamaliza matatizo ya maji nchini, lakini mpaka sasa imeshindwa kutekeleza ahadi hiyo.”

Mnyika anatoa kauli hiyo, ikiwa ni kilele cha maadhimisho ya wiki ya maji kitaifa; huku ujumbe wa mwaka huu, ukiwa “Maji kwa maendeleo endelevu.”

Maadhimisho ya mwaka huu yanafanyika mjini Musoma, mkoani Mara ambapo Rais Kikwete amepangwa kuhutubia taifa. Maadhimisho hayo ni ya mwisho kuhudhuriwa na Kikwete kama mkuu wa nchi.

Akiongea kwa uchungu, Mnyika amemtaka Waziri Mkuu wa Jamhuri, Mizengo Pinda, kutekeleze ahadi iliyotolewa na aliyekuwa waziri wa maji, Prof. Mark Mwandosya kwa niaba ya serikali kuwa katika kila mkutano wa Bunge kutawasilishwa taarifa ya mpango wa dharura kuhusu upatikanaji wa maji.

Mbali na ahadi ya rais, ilani ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2005, iliahidi ifikapo mwaka 2010 maji yangepatikana mijini ikiwemo jiji la Dar es Salaam kwa asilimia 90 na vijijini kwa asilimia 75. Amesema yote hayo yameshindwa kutekelezwa.

Wakati Rais Kikwete anaingia madarakani, Desemba mwaka 2005, upatikanaji wa maji ulikuwa ni asilimia 65. Lakini mwaka 2010 upatikanaji wa maji ulishuka hadi kufikia asilimia 55.

“Ili Rais asiendelee kuonekana dhaifu zaidi, walau kupitia siku hii ya maji awaagize watendaji katika ofsi yake watekeleze agizo alilowapa la kuitisha kikao cha kazi Ikulu kuhusu matatizo ya maji katika jiji la Dar es Salaam kama alivyoahidi,” amesema Mnyika.

Amesema zipo hatua zinazoweza kuchukuliwa katika kipindi cha miezi mitatu kuanzia sasa iwapo watakutana na kujadili udhaifu uliopo katika utekelezaji wa mpango maalum wa maji jijini Dar es Saam.

“Kwa kuwa nimeshamkumbusha yeye mwenyewe na wasaidizi wake mara kadhaa bila kikao hicho kuitishwa, ni wakati sasa wa wananchi wa Dar es Salaam kushiriki kumkumbusha kwa njia mtakazoona zinafaa,” ameeleza.

error: Content is protected !!