JOHN Mnyika, Naibu Katibu Mkuu (Bara) na Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Serengeti, John Heche wamezuiliwa polisi kwa madai ya kuwa wameshindwa kufuata taratibu za dhamana. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).
Viongozi hao wa Chadema pamoja na wengine walifika Kituo Kikuu cha Polisi kuitikia wito kama walivyotakiwa na jeshi hilo.
Walioachiwa kwa dhamana ni Mwenyekiti wa chama hicho, Freeman Mbowe, Naibu Katibu Mkuu (Zanzibar), Salum Mwalimu na Dk. Vicent Mashinji.
Mwalimu amesema Mnyika na Heche wamebaki polisi kwa maelezo kuwa wamekuwa wakikwepa taratibu za dhamana.
Heche na Mnyika hawakuripoti polisi Machi 16, 2018 huku chama hicho kikieleza kuwa moja ya sababu ya wabunge hao kutoripoti ni kutokana na kuhudhuria vikao vya kamati za Bunge mjini Dodoma.
Mbali na kina Mnyika na Heche kuzuiliwa kutokana na kutoripoti polisi kama walivyotakiwa, leo Mbunge wa Kawe, Halima Mdee na Ester Matiko hawajafika kutokana na kupata dharura.
“Mdee yupo nje ya nchi kwa matibabu na Ester Matiko yuko Dodoma kwa shughuli za kibunge amechelewa usafiri,” amesema Dk. Mashinji.
Jeshi la Polisi wametoa amri ya kukamatwa kwa Mdee na Matiko popote walipo kwa kosa la kutoripoti polisi leo kama walivyotakiwa kufanya hivyo.
Leave a comment