July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mnyika alianzisha bungeni

Aliyekuwa Mbunge wa Kibamba, John Mnyika

Spread the love

MBUNGE wa Ubungo, John Mnyika (Chadema) leo ametibua upya mgogoro wa upatikanaji wa mafuta katika vituo vya kuuza mafuta nchini. Anaandika Dany Tibason … (endelea).

Mnyika aliibua suala hilo ikiwa ni siku moja tu baada ya kusambaa kwa taarifa ya vituo vya mafuta kugoma kuuza mafuta hayo.

Hata hivyo Naibu Spika, Job Ndugai alimtaka Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Charles Mwijage kutoa ufafanuzi kuhusu taarifa ya Mnyika ya kuwepo kwa viashiria vya mgomo wa uuzaji wa mafuta.

Takribani siku 40 tangu Bunge lianze, Mnyika hakuwahi kuhudhuria ambapo jana ndio ilihudhuria.

Mnyika alianza moja kwa moja kwa kutoa hoja ya dharura ya kulitaka bunge lisitishe shughuli zake na kujadili jambo muhimu ambalo linaweza kuingiza taifa katika hali mbaya.

Amesema, kwa sasa kuna uwezekano mkubwa wa kukosekana kwa mafuta kutokana na kuwepo kwa viashiria vya baadhi ya wafanyabiashara wa mafuta kugoma kuuza mafuta.

“Mheshimiwa Naibu Spika nilikuwa naomba kutoa hoja ya dharura, leo hii kuna jambo kubwa ambalo linaweza kuliingiza taifa katika hali mbaya zaidi na mgogoro huo ni mafuta na ijulikane kuwa, mafuta ni uhai na mafuta ni maisha.

“Licha ya kumwagiza Naibu Spika juu ya masuala ya mafuta na kujibu hoja hiyo lakini nataka kusema, kuna uwezekano mkubwa wa kutokea mgomo, kwa siku ya jana mimi nilitoka Dar es Salaam na nilipita katika vituo zaidi ya vinane na vyote vilikuwa haviuzi mafuta.

“Hali hiyo inasababishwa na udhaifu wa serikali lakini pia mgogoro mkubwa na kubwa zaidi ni kutokana na kuporomoka kwa shilingi na uhifadhi wa mafuta,” amesema na kumtaka Naibu Spika akubaliane na hoja yake.

Hoja ya Mnyika iliungwa mkono na wabunge wote wa upinzani lakini Naibu Spika alitaka Naibu Waziri wa Nishati na Madini kujibu hoja hiyo.

Akijibu hoja hiyo Mwijage amesema, upatikanaji wa mafuta siyo tishio kwani kuna mafuta ya kutosha na zipo meli nyingine ambazo zinakuja kupakua mafuta.

Amesema, hifadhi ya mafuta ni kubwa kwa sasa na jambo muhimu ni kupata mafuta, kuyamudu na kupata mafuta ya kiwango.

“Kwa sasa tunayo mafuta mengi ambayo kwa makisio ya chini yanaweza kutumika kwa siku 14 na kwa makisio ya juu yanaweza kutumika kwa siku 40.

“Pamoja na hayo ni kweli jana  kuna vituo 8 ambavyo havikuweza kuuza mafuta lakini na hali hiyo inaendelea kuchunguzwa kwani kuna uwezekano vituo vingine havikuwa na mafuta kabisa.

Akiendelea kuelezea suala hilo Mwijage amesema, wafanyabiashara wote ambao watakuwa wamebainika kufanya makusudi kutouza mafuta ni wazi watatozwa faini ya Sh. Milioni 20 au kufungiwa vituo vyao na kuporwa leseni zao.

“Ninaomba wabunge mtulie na sasa nimuombe Mh, Tundu Lissu pamoja na mwanasheria wa serikali kutusaidia kuwashitaki wale wote ambao wataonekana kukaidi sheria ya uuzaji wa mafuta makusudi wakati mafuta yapo ya kutosha,” amesema.

Spika Ndugai aliwataka wabunge hao kuwa wavumilivu ili kuona kama mgogoro huo utaendelea.

“Natambua tatizo hilo lipo na kubwa lakini nina uhakika litaisha kesho na tatizo hili ni kutokana na Mamlaka ya Uthibiti wa Nishati na Maji (EWURA) kuhakikisha wanapanga bei ili kumaliza mgogoro huo.

error: Content is protected !!