KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo-Chadema Taifa, John Mnyika mapema leo amefika msibani nyumbani kwa kada wa chama hicho aliyefia vitani nchini Ukraine akiipigania Urusi, Nemes Tarimo na kuacha ujumbe. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)
Katika ujumbe wake Mnyika ameonesha namna chama chake kinavyotambua mchango wa Nemes katika mapambano ya haki, demokrasia na maendeleo ya wananchi.
“Rest in peace mpambanaji Nemes Raymond Tarimo, nilipokea kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo chako, umetangulia mbele za haki katika umri mdogo. Tukiwa bado tunatamani mchango wako katika mapambano ya kutafuta uhuru, haki, demokrasia na maendeleo ya watu Chadema katika jimbo la Kibamba linatambua mchango wako wakati wa mchakato wa kura za maoni ya uteuzi wa mgombea ubunge jimbo la Kibamba katika uchaguzi wa mwaka 2020 ni sala yangu kuwa Mwenyezi Mungu akupe rehema na neema ya kupata mwanga wa milele. Upumzike kwa Amani,” ameandika nyika katika kitabu hicho.
Naye Mwenyekiti wa Chadema kata ya Saranga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bawacha mkoa wa Ubungo, Magreth Kyai, amesema msiba huo umewagusa sana kwasababu Nemes alikuwa mtu wa karibu mwenye kujali wanachama, alipenda siasa na alipenda chama chake cha Chadema.
Amesema ushiriki wa Chama katika msiba huo ni kubwa kwani Katibu Mkuu amefika na kutoa ujumbe na pia viongozi wa chama mkoa wa Ubungo watafika na wametoa rambirambi zao kama chama.
Mwili wa Nemes umewasili leo kutokea nchini Urusi na utaagwa nyumbani kwake Saranga na baadae kusafirsihwa kwenda mkoani Mbeya kwa maziko
Leave a comment