July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mnapanga kumng’oa Meya Kigoma, thubutuni – Zitto

Spread the love

MKAKATI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), kutumia hila kumng’oa Meya wa Manispaa ya Kigoma, Ujiji, Hussein Ruhava umetua kwa Zitto Kabwe. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Hata hivyo, Zitto ambaye ni mwanasiasa imara wa upinzani na Kiongozi Mkuu wa Chama cha ACT-Wazalendo, amesema ‘thubutuni.’

Jana tarehe 9 Januari 2020, CCM wametangaza kumwondoa Isaya Mwita, aliyekuwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam (Chadema), bila kujali kukamilika kwa akidi ya wajumbe wa mkutano uliotumika kumwondoa madarakani.

Mwanasiasa huyo mwenye ushawishi mkubwa wa kisiasa mkoani Kigoma, ametoa onyo hilo tarehe 9 Januari 2020, saa kadhaa baada ya CCM kutangaza kumng’oa Isaya kwa hila.

Zitto ameeleza kuwa, anasubiri kwa hamu watu wanaotaka kumng’oa Meya wa Kigoma, Ujiji anayetokana na chama chake cha ACT-Wazalendo.

Kiongozi huyo wa ACT-Wazalendo ameeleza kuwa, CCM isifikiri Jiji la Dar es Salaam ni sawa na Kigoma.

“Kila nikionana na watu wa CCM, wananiambia Namba 1 kaamua kuwa lazima ushindwe Kigoma Mjini. Hata ukipata kura asilimia 200 hawakutangazi.

“Mimi hucheka na kuwaambia, watu wa Kigoma ni werevu sana. Sasa wanataka kumtoa Meya wa Kigoma, Ujiji kama Dar es Salaam. Watajua Kigoma sio Dar es Salaam. Tunawasubiri,” amesema Zitto.

Amesema, CCM haitafanikiwa kumng’oa Ruhava, kwa kuwa Baraza la Madiwani la Kigoma Ujiji lina madiwani wengi wa ACT-Wazalendo, kuliko wa chama hicho.

Aidha, Zitto amelaani kitendo cha Meya Mwita kuondolewa madarakani, akidai kwamba kitendo hicho ni kinyume na sheria.

“Ninalaani vikali kuondolewa mamlakani kwa Meya wa Jiji la Dar es Salaam, Isaya Mwita kinyume cha Sheria na Kanuni za Serikali za Mitaa. Ninatuma salamu za mshikamano kwa Mwenyekiti wa Chadema,” amesema Zitto.

error: Content is protected !!