April 14, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mlenga shabaha (Sniper) atinga kwenye kesi ya viongozi Chadema

Viongozi wa Chadema wakiwa Mahakamani Kisutu

Spread the love

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu imeendelea kusikiliza ushahidi wa shahidi wa nne kwenye kesi  inayowakabili viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendelea (Chadema), ambapo shahidi amekiri kuwa yeye ni mlenga shabaha na amegoma kutaja kazi mahususi iliyompeleka kwenye tukio la maandamano ya viongozi na wafuasi wa Chama hicho. Anaripoti Faki Sosi … (endelea).

Kesi hiyo ya Uchochezi namba  112 ya mwaka 2018, inayowakabiri viongozi hao wa Chadema ambao inadaiwa tarehe 16 Februari, 2018 walifanya maandamano yasiyo halali.

Leo tarehe 31 Mei 2019, Mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba upande wa Serikali uliongozwa na wakili Faraja Nchimbi, Paul Kadushi, Wankyo Simon na Jackline Wantori ulimleta shahidi wao mahakamani hapo aliyejitambulisha kuwa ni askari polisi H7856 PC Fikiri Mgeta mwenye miaka 28.

Katika kesi hiyo upande wa utetezi umewakiliswa na Wakili Pater Kibatala, Jeremiah Mtobesya, John Mallya, Dickson Matata na Hekima Mwasipu.

Mtuhumiwa namba moja kwenye kesi hiyo ni Freeman Mbowe, Mwenyekiiti wa Chama hicho, Vincent Mashinji, Katibu Mkuu wa Chama hich, John Mnyika, Naibu Katibu Mkuu Bara, Salum Mwalimu, Naibu Katibu Mkuu Z’bar.

Wengine ni Ester Matiko Mbunge wa Tarime vijijini, Ester Bulaya Mbnge wa Bunda Mjini, Halima Mdee, Mbunge wa Kawe, Peter Msigwa Mbunge wa Iringa Mjini, na John Heche, Mbunge wa Tarime Vijijini.

Yafuatayo ni mahojiana kati ya Wakili wa utetezi, Kibatala na Shahidi PC Fikiri:-

Wakili Kibatala: Ni sahihi kwamba utambuzi wako kwenye jeshi la Poilisi wewe ni mlenga shabaha?

Shahidi:  Ni sahihi.

Wakili Kibatala: Na ni sahihi kwamba hiyo kazi yako ya mlenga shabaha imeleza kwenye (ID2) kuwa wewe ni Mlenga Shabaha Mahususi?

Shahidi: Sio kweli.

Wakili Kibatala: Unaitambua ID2 kuwa ni PF3. Kwenye (ID2) utambuzi wa kuwa mlenga shabaha kweli au sio kweli?

Shahidi: Sio kweli.

Wakili Kibatala: Shahidi ulizungumzia kazi iliyokuelekea kuifanya pale Mkwajuni?

Shahidi: Nilizungumzia.

Wakili Kibatala: Ulisema ulikwenda kupiga mabomu, kulinda gari au kazi gani mahususi?

Shahidi: Nilisema kuwa nilikwenda kuongeza nguvu.

Wakili Kibatala: Kuongoza nguvu ni kupiga mabomu, kupiga risasi viongozi wa Chadema au nguvu ipi?

Shahidi: Kupiga mabomu kitu kingine mimi nilikwenda kulinda amani pale.

Wakili Kibatala: Je ulisema kazi gani mahususi iliyokupeleka pale?

Shahidi: Nilikwenda kulinda amani.

Wakili Kibatala: Kwa kufanya kitu gani kushika bendera au kufanya nini?

Shahidi: Rudia swali.

Wakili Kibatala: Ulisema kazi mahususi uliyokwenda kufanya pale?

Shahidi: Nilisema kulinda amani.

Wakili Kibatala: Kazi ipi mfano mimi hapa tumekuja na mawakili wenzangu kuendesha kesi lakini sasa nakuuliza wewe maswali wewe ulisema kazi gani?

Hakimu Simba: Kama hajakuelewa unaweza kubadilisha swali.

Wakili Kibatala: Sina haja ya kubadilisha swali wala sihitaji mtu kusimama kuingilia wakati unaongozwa na wakili Nyantori ulielekezwa kazi gani ulikwenda kufanya?

Shahidi: Nilisema kwamba nilienda kulinda amani.

Wakili Kibatala: Kazi mahususi uliitaja?

Shahidi: Niliitaja.

Wakili Kibatala: Kwa mfano ulisema kwamba wewe ulikuwa unapiga mabomu?

Shahidi: Sikusema.

Wakili Kibatala: Ulisema kama ulipiga risasa?

Shahidi: Sikusema.

Wakili Kibatala: Ulizumgumzia kama ulishika Ilani?

Shahidi: Sikusema.

Wakili Kibatala:  Ulisema kama ilikuwa dereva?

Shahidi: Sikusema.

Wakili Kibatala: Wakati unatoa ushahidi wako ulisema Ilani imetamkwa mara ngapi?

Shahidi: Sikuzungumzia hiyo.

Wakili Kibatala: Unafahamu Ilani ni tamko halali la kisheria linatakiwa litamkwe mara ngapi?

Shahidi: Siwezi kusema.

Wakili Kibatala: Unafahamu au haufahamu?

Shahidi: Sifahamu.

Wakili Kibatala: Wakati unatoa ushahidi wako ulizungumzia kunyanyuliwa kwa kitambaa chekundu?

Shahidi: Nilizungumzia.

Wakili Kibatala: Mwambie hakimu hiko kitambaa kilinyanyuliwa na nani?

Shahidi: Askari.

Wakili Kibatala: Ulimwambia Hakimu hiko kitambaa kilinyanyuliwa na nani?

Shahidi: Mheshimiwa hakimu kitambaa kilinyanyuliwa na askari.

Wakili Kibatala: Hujanielewa wakati unatoa ushahidi hapo awali hayo maneno kwamba kitambaa kilinyanyuliwa  ulisema hujasema?

Shahidi: Nilisema.

Wakili Kibatala: Wakati unatoa ushahidi wako uliyataja majina ya askari waliokuwa wakinyanyua kitambaa chekundu cha Ilani?

Shahidi: Hapana.

Wakili Kibatala: Kitambaa cha Ilani kinakuwa na maneno ya kisheria kweli au sio kweli?

Shahidi: Kweli.

Wakili Kibatala: Uliongozwa kuyarudia maneno ya kwenye Ilani?

Shahidi: Sikuyarudia.

Wakili Kibatala: Maneno haya ya kwenye Ilani yalishikwa na nani?

Shahidi: Askari wenyewe.

Wakili Kibatala: Ni nani?

Shahidi: Siwezi kuwataja.

Wakili Kibatala: Huwezi kuwataja hutaki au hujui?

Shahidi: Sikumbuki.

Wakili Kibatala: Ni nani anatakiwa kisheria akisimamie kile kitambaa cha Ilani?

Shahidi: Sifahamu.

Wakili Kibatala: Shahidi mawakili tulikwenda eneo la tukio tunalifahamu ulisema kwamba umekatisha vichochoroni ukatokea eneo la tukio ulitaja huo mtaa au hukutaja?

Shahidi: Sikutaja.

Wakili Kibatala: Hizo njia za pembeni ulizizungumzia kwa kuchora picha angalau na sisi tuzijue?

Shahidi: Nilizungumzia.

Wakili Kibatala: Hizo barabara zote zina majina  umezitaja au hujazitaja?

Shahidi: Sijazitaja.

Wakili Kibatala: Kulikuwa na msululu mrefu kutoka Mkwajuni kwenda kigogo na kutoka kigogo kuja Mkwajuni ni sahihi?

Shahidi: Sahihi.

Wakili Kibatala: Hapo  jerani na Mkwajuni  kulikuwa na makutano ya barabara?

Shahidi: Hapakuwa.

Wakili Kibatala: Kulikuwa na barabara ambazo zilingia kwenye barabara kuu?

Shahidi: Hazikuwepo.

Wakili Kibatala: Nikikuuliza kuhusu mmepenya kwenye barabara gani itakuwa tunapoteza muda.

Wakili Kibatala: Shahidi uliongozwa kuwataja Mbowe, Mdee, na Mwalimu. Mwambia Hakimu kuwa ulikumbukuka kutambua nguo za Mbowe?

Shahidi: Hapana.

Wakili Kibatala: Pengine kwa wengine jibu litakuwa hivyo hivyo.

Nchimbi amesimama ameeleza mahakama kuwa wakili anamlisha maneno shahidi.

Hakimu Simba: Endelea.

Wakili Kibatala: Ulizungumza kuhusu nguo za Salum Mwalimu?

Shahidi: Sikuzungumzia.

Wakili Kibatala: Ulizungumia kuhusu nguo za washtakiwa wengine?

Shahidi: Sikutaja.

Wakili Kibatala: Ni sahihi kwamba washtakiwa wengine wote ukitoa hawa wanne uliwatambua hapa kwenye mahakamani?

Shahidi: Sahihi.

Wakili Kibatala: Bila shaka hadi mabomu yanaanza kupigwa wewe ulikuwa hujaumizwa?

Shahidi: Ni sahihi.

Wakili Kibatala: Mabomu wakati yanapigwa viongozi hawa walikuwa wakihamasishana wasonge mbele?

Shahidi: Sahihi.

Wakili Kibatala: Kuna mahali ulisema Mbowe alikimbia?

Shahidi: Sio sahihi.

Wakili Kibatala: Kwa muda gani wewe kabla ya kuumia mabomu yalipigwa?

Shahidi: Kama dakika 5.

Wakili Kibatala: Ni sahihi kuwa hakuna mahali popote ulipozungumzia kukimbia kwa Mbowe hadi kudondosha miwani yake?

Shahidi: Sahihi.

Wakili Kibatala: Hapa Mahakamani asimilia kubwa waliokuja ni wafuasi wa Chadema mwambie hakimu kwamba wengi wao walivaa au hawakuvaa nguo za Chadema?

Shahidi: Siwezi kuzungumzia.

Wakili Kibatala: Shahidi kuwa kama hapa kwenye umati huu kama kuna mtu amevaa mzura unaweza kumkalili?

Shahidi: Sahihi.

Wakili Kibatala: Mwambie Hakimu kama uliwaona watu waliovaa mizura kwenye maandamano yale?

Shahidi: Sikumbuki.

Wakili Kibatala: Kwa ufahamu wako wewe kuna tukio la kutisha kuna hatari watu wameandamana watu wamejaa kwenye magari ni kitu cha kawaida watu kukaa ndani ya magari?

Shahidi: Siwezi kuzungumzia.

Kadushi: (kasimama) Ushahidi upo wa kuona upo wa kusikia na kama shahidi anahitajika kutoa ushahidi wa maoni.

Wakili Kibatala: Shahidi nakuuliza hali ya kawaida kwa sababu ulisema watu walikuwa wamehamaki unataka kuiambia mahakama iamini kuwa watu wasingeweza kushuka?

Shahidi: Kwa mazingira ya eneo la tukio sio sahihi watu kushuka kwenye gari.

Wakili Kibatala: Shahidi hebu tusaidie kuna mtu yoyote aliyekuja kuomba akingwe ili mazara yasimtokee?

Shahidi: Hakuna.

Wakili Kibatala: Uliambiwa au hukuambiwa kuwa kuna moja ya shtaka hapa tukio hilo ilisababisha mtu afariki?

Shahidi: Sikuambiwa.

Wakili Kibatala: Afande Ngichi au Askari yoyote alipata nafasi ya kuwasiliana na waandamanaji kujua wanakwenda wapi?

Shahidi: Sifahamu.

Wakili Kibatala: Wakati afande Ngichi anatoa Ilani na anawaamuru watu wa mabomu wasonge mbele ulishuhudia?

Shahidi: Ndio.

Wakili Kibatala: Uliweza kufahamu hawa viongozi labda walikuwa wakiinda makwao au kwenda kunywa bia?

Shahidi: Sikuweza kufahamu.

Wakili Kibatala: Ushahidi wako ni kwamba barabara ilikuwa imefungwa hawa waandamanaji walikuwa katikati?

Shahidi: Ndio zilifungwa kwa sababu ya maandamano?

Wakili Kibatala: Labda kwa vile njia zimefungwa na Afande Ngichi aliwaelekeza piteni njia hii?

Shahidi: Hakusema.

Wakili Kibatala: Kuna mahala popote afande Ngichi alisema wekeni mawe chini?

Shahidi: Hakusema.

Wakili Kibatala: Wewe unafahamu hao watu 500 au 600 unafahamu wanaishi wapi?

Shahidi: Sifahamu.

Wakili Kibatala: Wakati watu wanatamka hatupo kuna tatizo lolote kisheria?

Shahidi: Inategemea kwenye tukio gani.

Wakili Kibatala: Watu waliokuwa wameandamana wameambiwa watawanyike hawakuambiwa watawanyike waeleke wapi wanaimba hatupoi wanatoka jasho kuna tatizo?

Shahidi: Inategemea na hali ya amani.

Wakili Kibatala: Pamoja na kuwa hatujui kuwa ulikwenda kwa shughuli gani ingawa tunajua kuwa  wewe ni mlengaji shabaha ni sahihi shahidi kamera ni sehemu ya vifaa vya kipolisi?

Shahidi: Siwezi kuzungumzia.

Wakili Kibatala: Shahidi hujui au hutaki?

Shahidi: Sijui.

Wakili Kibatala: Uliwahi kuhojiwa kuhusu kupigwa jiwe.

Shahidi: Sijawahi kuhojiwa.

Wakili Kibatala: Nani aliyekupiga jiwe kati ya watuhumiwa hawa tisa?

Shahidi: Sifahamu .

Wakili Kibatala: Ukitoa tisa ni nani mwengine unayeweza kufahamu aliyekupiga jiwe?

Shahidi: Siwezi kumfahamu.

Kibatala ameomba kuahilishwa kwa kesi hiyo kutokana na muda kuwa mchache na kwamba kuna baadhi ya watuhumiwa wamefunga (mfungo wa Ramadhan).

Hakimu Simba amehailisha shauri hilo mpaka tarehe 4 na 5 Juni mwaka huu kwa ajili ya kuendelea usikilizwaji.

error: Content is protected !!