August 15, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mkwara wa Magufuli wamkimbiza Kimbisa

Spread the love

BODI ya Uhuru Media Group, wasimamizi wa vyombo vya habari ambavyo ni mali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ikiwemo gazeti la Uhuru, Mzalendo na redio Uhuru imejiuzulu uongozi wake leo ikiwa ni siku tatu tu tangu kubainika kwa ‘madudu’ mengi katika uendeshaji wa vyombo hivyo vya habari, anaandika Charles William.

Bodi hiyo iliyokuwa chini ya uongozi wa Adam Kimbisa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Dodoma, ndiyo yenye jukumu la kusimamia na kushauri juu ya uendeshaji wa vyombo hivyo vya habari.

Mwanzoni mwa wiki hii, Rais John Magufuli, Mwenyekiti wa CCM taifa, alitembelea ofisi za Uhuru Media Group zilizopo umbali wa mita takribani 30 kutoka jengo la ofisi ndogo za CCM, Lumumba na kubaini ‘madudu’ mengi ikiwemo wafanyakazi kutolipwa mishahara kwa miezi saba.

Wakati wafanyakazi wa vyombo hivyo, wakidai malimbikizo ya mishahara kwa miezi saba, inayofikia jumla ya Sh. 609 milioni, Rais Magufuli pia alibaini kuwa, mtambo wa kuchapishia magazeti ambao ni mali ya kampuni hiyo umeuzwa ‘kinyemela’ na kwa bei ya hasara.

Rais Magufuli pia alielezwa kuwa, vyombo hivyo vya habari mali ya CCM, vinadai fedha kutoka taasisi mbalimbali za Serikali ikiwemo wizara, kiasi cha zaidi ya 1 bilioni, kama gharama za matangazo, hali inayovifanya vyombo hivyo viwe na hali mbaya.

Barua ya kujiuzulu iliyoandikwa na Adam Kimbisa, mwenyekiti wa bodi ya Uhuru Media Group imewasilisha leo kwa Rais Magufuli ambaye ndiye mwenyekiti wa chama hicho na nakala kukabidhiwa kwa Abdurahman Kinana, Katibu Mkuu wa chama hicho.

Hata hivyo, taarifa iliyotolewa jioni ya leo na Christopher Ole Sendeka, Msemaji wa CCM taifa, haikuweka wazi sababu za bodi hiyo kujiuzulu katika kipindi hiki ambacho inakabiliwa na tuhuma za kushindwa kusimamia uendeshwaji vyombo hivyo vya habari.

Hata hivyo, hatua hiyo inaweza kutafsiriwa kama ni kukiri udhaifu wa bodi hiyo katika kuiendesha Uhuru Media Group.

Itakumbukwa kuwa baada ya Rais Magufuli baada ya kupata malalamiko ya wafanyakazi wa kampuni hiyo, alimtaka Kinana kuhakikisha wafanyakazi hao wanalipwa ndani ya mwezi huu, lakini akiahidi kufanyia kazi uuzaji kinyemela wa mtambo wa kuchapishia magazeti.

error: Content is protected !!