June 22, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mkwamo wa kiuchumi Tanzania sasa dhahiri

Spread the love

MIEZI kumi tangu kuingia kwa utawala wa awamu ya tano, chini ya Rais John Magufuli, hali ya kiuchumi hapa nchini inazidi kudorora kwa kasi kadri muda unavyoenda, huku sekta muhimu kiuchumi nazo zikidorora kwa kasi ya ajabu, anaandika Charles William.

Wakati Mamlaka ya Mapato hapa nchini (TRA), ikijipongeza kwa kukukusanya shilingi 1.158 trilioni kama mapato ya mwezi Agosti na hivyo kuvuka lengo lao la kukusanya kiasi cha shilingi 1.152 trilioni, hali ni mbaya kwenye sekta zinazogusa maisha ya kila siku ya wananchi.

Sekta ya ujenzi ambayo ndiyo yenye mnyororo mrefu zaidi kiuchumi hapa nchini, inaonekana kuporomoka kwa kasi katika kipindi cha utawala wa Rais Magufuli, jambo linaloathiri wananchi wa kipato cha chini kwa kiasi kikubwa.

Ripoti ya Benki Kuu ya Tanzania (BoT) katika robo ya mwisho ya mwaka 2015 ilionesha kuwa sekta ya ujenzi inakua kwa 13.8% lakini ukuaji wa sekta hii katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 ni 4.30% pekee, ikiwa imeporomoka kwa karibu 10%.

Kwa kawaida, ukuaji wa sekta ya ujenzi husaidia kukua kwa uchumi wa wananchi wengi sana, ikiwemo wahandisi, mafundi ujenzi, wauzaji wa saruji, wabeba mizigo, wabeba zege, wauzaji wa chakula wakiwemo Mama’ntilie, madereva, wafyatuaji wa matofali na wengineo wengi.

Kuporomoka kwa sekta hii kwa zaidi ya asilimia 10, kunaashiria kuwa idadi ya watu wanaojenga imepungua kwa kiasi kikubwa, ikiwa ni kutokana na ugumu wa maisha au kutokuwepo uhakika wa wapangaji wapya. Mzunguko wa fedha umepungua na hili ni pigo kubwa kwa wananchi masikini.

Pengine kuporomoka kwa sekta hii ya ujenzi na hatimaye mzunguko mdogo wa fedha ndiyo kumesababisha Rais Magufuli kusikika wiki iliyopita akilalamika kuwa, kuna watu wanaoficha fedha ndani na kutishia kuchapisha noti mpya!

Sekta ya usafirishaji nayo imeporomoka kutoka kukua kwa 14.50% robo ya mwisho ya 2015 mpaka kukua kwa 7.9% robo ya kwanza ya 2016, ikiwa ni kuporomoka kwa 7% katika kipindi cha miezi 6 tu ya kwanza ya utawala wa Rais Magufuli.

Chama cha Usafirishaji wa Mizigo Tanzania (TATOA) kinachomiliki wastani wa magari 23,000 ya kusafirisha mizigo kimeripotiwa kueleza kuwa, 60% ya magari yao kwa sasa hayafanyi kazi kutokana na uhaba mkubwa wa mizigo bandarini.

Takwimu hizi zinamaanisha kuwa zaidi ya madereva na wasaidizi wao (utingo) 27,600 wa malori wanakosa kazi kwa sasa. Jambo linaloathiri familia zao kwa kiasi kikubwa lakini pia serikali ikikosa mapato makubwa kutokana na kupungua kwa mauzo ya mafuta ya magari.

Serikali hukusanya wastani wa karibu Shilingi 650/- katika kila lita moja ya mafuta ikiwa ni makato ya kodi.

Wakati hali ikiwa hivi, taarifa za (BoT) zinadokeza zaidi kuwa, kwa robo ya mwisho ya mwaka 2015 (Oktoba – Desemba 2015), kasi ya ukuaji wa Pato la Taifa ilikuwa 9% lakini katika robo ya kwanza ya mwaka 2016 (Januari – Machi 2016) ilishuka hadi kufikia 5.5%.

Siyo ripoti za BoT pekee zinazoonesha hali mbaya ya kiuchumi hapa ncgini. Ripoti za Benki ya Dunia (WB), zinaeleza pia kuwa Tanzania ni nchi ambayo deni lake la taifa linakua kwa kasi zaidi katika ukanda wa Afrika Mashariki.

Deni la taifa la Tanzania ni 40% ya pato la taifa hali inayoliweka taifa pabaya zaidi kiuchumi kulinganisha na deni la taifa la Kenya ambalo ni 25% ya pato la taifa lao na deni la taifa la Uganda ambalo ni 20 ya pato la taifa hilo.

Pia Tanzania imeendelea kukopa kwa kasi zaidi kwani katika kipindi cha robo mwaka tu cha utawala wa Rais Magufuli tayari serikali yake imekopa zaidi ya 900 milioni dola za kimarekani ambazo ni zaidi ya Shilingi 2 trilioni za kitanzania.

error: Content is protected !!