March 9, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mkuu wa Mkoa atimua uongozi Ndanda FC

Spread the love

MKUU wa mkoa wa Mtwara, Gilasius Byakanwa ameamua kuuweka pembeni uongozi wa klabu ya Ndanda FC inayoshiriki Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kushindwa kuiongoza timu hiyo katika msimu huu 2018/19. Anaripoti Kelvin Mwaipungu … (endelea).

Kiongozi huyo ameamua kuchukua maamuzi hayo kufuatia timu hiyo kushindwa kulipa gharama za hoteli mkoani Singida walipokwenda kwa ajili ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Singida United na kushindwa kuwa hata na pesa ya mafuta ya kuisafirisha timu kurudi mkoani Mtwara.

“Huwezi kuwa na viongozi ambao wakikutana hawawezi hata kununua maji kwaajili ya wachezaji au huwezi kuwa na viongozi kwenye timu ambao wakikutana wanafikilia kile kilichoingia kwa ajili ya maslahi yao wenyewe,” alisema Byakanwa.

Baada ya kuutimua uongozi huo Byakanwa ameunda safu mpya ya uongozi ambao itaiendesha klabu hiyo mpaka msimu huu wa ligi utakapomalizika ambapo mwenyekiti wake atakuwa Laurent Welema huku wajumbe ni Stanley Milanzi, Athuman Kambi, Raymond Kasuga, Joseph Beneza, Badwin Masawe, Mohammed Lemtura, Mohammed Nassoro na Said Ally.

Aidha mkuu huyo wa mkoa aliongezea ya kuwa kama msanii wa muziki wa kizazi kipya, Rajab Abdul ‘Harmonize’ atakubali naye ataingia katika safu hiyo ya uongozi.

Ikumbukwe Harmonize ndiye aliyeisaidia timu hiyo kiasi cha Sh. 3 milioni ili waweze kulipa deni walilokuwa wakidaiwa hotelini timu ilivyokuwa mkoani Singida sambamba na kuweka mafuta gari ili waweze kurejea Mtwara.

error: Content is protected !!