Spread the love

MKUU wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo, anatarajia kumaliza utumishi wake ndani ya jeshi hilo, mwishoni mwa Juni, 2022. Anaripoti Mwandishi Wetu, Zanzibar…(endelea).

Hayo yamebainika leo Jumatu, tarehe 6 Juni 2022, wakati Jenerali Mabeyo alipokwenda kumuaga Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi, Ikulu visiwani humo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Idara ya Mawasiliano ya Ikulu ya Zanzibar, Rais Mwinyi amempongeza Jenerali Mabeyo, kwa utumishi wake uliotukuka katika kipindi chote alichokuwepo ndani ya jeshi hilo.

Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania, Jenerali Venance Mabeyo (kulia) akiwa na Rais wa Zanzibar, Dk. Hussein Mwinyi (kushoto) alipofika Ikulu, Zanzibar kumuaga

 

“Katika maelezo yake, Rais Dk. Mwinyi alimuelezea Jenerali Mabeyo, kwamba ni kiongozi ambaye alifanya kazi zake vyema katika Jeshi hilo na alimpa ushirikiano mkubwa yeye na viongozi wenzake wakati akiwa Waziri wa Ulinzi, hatua ambayo ilimuwezesha kutekeleza mambo mengi ndani ya Jeshi hilo,” imesema taarifa ya Ikulu ya Zanzibar.

Kwa upande wake Jenerali Mabeyo, alimshukuru Rais Mwinyi kwa ushirikiano aliompatia tangu akiwa Waziri wa Ulinzi hadi hivi sasa akiwa Kiongozi Mkuu wa Zanzibar.

“Nakutakia afya njema na maisha marefu Mheshimiwa Rais pamoja na familia yako….nathamini sana ushirikiano ulionipa katika kipindi chako cha uongozi tokea ukiwa Waziri wa Ulinzi hadi leo hii, ahsate sana,” amesema Jenerali Mabeyo.

Jenerali Mabeyo amesema kwamba, katika uongozi wake Rais Dk. Mwinyi, akiwa Waziri wa Ulinzi, aliweza kutatua changamoto kadhaa sambamba na kulifanyia mambo mengi Jeshi hilo hatua ambayo imepelekea viongozi wa Jeshi hilo waendelee kufuata nyayo zake.

Jenerali Mabeyo anayemaliza muda wake mwishoni wa Juni, mwaka huu, alishika wadhifa wa Mkuu wa Majeshi wa nane, Februari 2017, baada ya kuteuliwa na aliyekuwa Rais wa Awamu ya Tano, Hayati John Magufuli.

Jenerali Mabeyo alijunga na Jeshi la Ulinzi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), tarehe 1 Januari 1979, na kuhudhuria kozi mbalimbali ndani na nje ya nchi, ikiwemo Kenya, India, Canada na Marekani.

Kwa mujibu wa tovuti ya JWTZ, Jenerali Mabeyo ametunukiwa medali mbalimbali, ikiwemo ya miaka 20 ya utumishi wa JWTZ, utumishi mrefu, miaka 40 ya JWTZ, utumishi uliotukuka.

Medali nyingine ni ya Comoro na Anjouan, medali ya miaka 50 ya uhuru, medali ya miaka 50 ya muungano na miaka 50 ya JWTZ.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *