December 1, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mkuu Chuo Uhasibu Arusha amlilia Rais Samia uhaba wa wahadhiri

Spread the love

 

MKUU wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka amemuomba Rais Samia Suluhu Hassan kutupia jicho elimu ya juu kwani ina upungufu mkubwa wa wahadhiri changamoto ambayo inazidi kuvitesa vyuo vingi nchini. Anaripoti Mwandishi Wetu, Arusha … (endelea).

Prof. Sedoyeka ametoa kauli hiyo leo tarehe 22 Novemba, 2021 jijini Arusha wakati akihutubia mahafali ya pili kwa maofisa wapya 118 waliotunukiwa kamisheni na Rais Samia katika Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli.

Kati yao wahitimu 56 ni wa kundi la jeshi la anga wakati 61 wamehitimu shahada ya sayansi ya kijeshi inayotolewa na Chuo cha Mafunzo ya Kijeshi Monduli kwa kushirikiana na Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA).

Aidha, akizungumzia changamoto hiyo ya uhaba wa wakufuzi au wahadhiri katika vyuo vikuu nchini, Prof. Sedoyeka amesema, “kwa miaka kadhaa sekta hii haijaajiri… tunashukuru juzi ulitoa kibali kwa ajili ya walimu wa sekondari na msingi lakini tunaomba sasa utuangalie kwa jicho la kipekee elimu ya juu, kuna upungufu mkubwa sana wa walimu,” amesema.

Pia ametoa wito kwa Serikali kuiga mfumo wa Serikali ya China ambayo baada ya vita ya pili ya dunia iliamua kufanya mapinduzi makubwa kwenye sekta ya elimu.

Amesema ni wakati muafaka kwa Serikali kuangalia sera ya viwanda na sera ya elimu na kuziunganisha ili kuendana na uhalisia wa sasa.

“Serikali ijenge shule za ufundi katika kila tarafa, hii inawezekana kwa kujenga karakana moja kwenye shule mojawapo ya kata katika tarafa hiyo kutokana na shughuli za kiuchumi.

“Kwa mfano kama eneo lina mbao nyingi tukiunda karakana ya useremala na mwaka unaofuata karakana nyingine. Ikifika mwaka 2025 shule itakuwa na karakana tano au sita na vijana wa eneo hilo watakuwa wamejifunza,” amesema.

Mkuu wa Chuo cha Uhasibu Arusha (IAA), Prof. Eliamani Sedoyeka

Pia ametoa wito kwa serikali kujenga vyuo vya ngazi ya Stashahada (diploma) katika kila wilaya na Shahada katika kila mkoa ili kuwezesha viwanda kuwatumia wanafunzi katika tafiti na bunifu mbalimbali badala ya viwanda hivyo kuwa na idara zinazohusu masuala hayo.

“Zile kazi zitaletwa chuoni moja kwa moja hivyo vijana wanajifunza kivitendo na baadaye wakitoka wanaenda kwenye kazi moja kwa moja.

“Hii itajengea vijana kuwa na ujuzi kuunda vitu mbalimbali na baadaye kujiajiri wataweza kuunda viwanda vidogo na kuvutia wawekezaji katika wilaya husika.

Rais Samia Suluhu Hassan

“ Pia nchi itavutia sana wawekezaji kwani wakija watakuwa na uhakika wa rasilimali watu, pia itapunguza vijana kuhamia mijini jambo ambalo ni tatizo linalotoa nguvu kazi maeneo ya vijiji na kuchelewesha maendeleo katika eneo lile,” amesema.

Aidha, ametoa wito kwa wahitimu hao kutumia elimu waliyoipata kujenga nchi katika misingi ya endelevu, haki na kuwatumikia watanzania kwa moyo na werevu mkubwa pasipo kujali dini ukabila.

error: Content is protected !!