MKUTANO wa kwanza wa kihistoria uliojumuisha mahakama ya haki barani Afrika na mbili za kikanda umemalizika leo kwa matumaini ya kupatikana msingi wa kuwezesha maamuzi ya mahakama hizo kutekelezwa na Serikali husika. Anaripoti Jabir Idrissa, Zanzibar … (endelea).
Akifunga mkutano huo kwenye Hoteli ya Verde, mjini Zanzibar, Waziri wa Sheria na Katiba wa Zanzibar, HAROUN ALI SULEIMAN alisema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar inatambua mchango mkubwa wa mahakama hizo zikiongozwa na ile ya Bara la Afrika – Mahkama ya Haki za Binaadam na Watu – na inafurahi kuamua kuichagua Zanzibar kuwa mwenyeji wa kwanza wa mkutano huu.
Waziri Haroun ambaye ni mwanataaluma ya ualimu amesema Serikali inajali haki za watu wakiwemo wale wa makundi maalum na inachukua kila hatua kuhakikisha watu wote wanazifaidi haki hizo.
Ametilia mkazo umuhimu wa kuwepo mfumo mahsusi wa kuwezesha Serikali katika nchi wanachama wa mahkama hizo kutekeleza maamuzi yanayotolewa kutokana na kesi zinazofikishwa na wananchi wa barani Afrika.
Rais wa Mahkama ya Haki za Binaadam na Watu, Jaji Imani Aboud akitoa maelezo kabla ya kumkaribisha Waziri Haroun, amesema ana matumaini lengo la mkutano wao wa siku tatu limefikiwa na kwamba maazimio yaliyopo yataonesha dira ya kuondokana na utamaduni wa nchi wanachama kupuuza wajibu wa kutekeleza maamuzi ya mahkama hizo ambazo zimeanzishwa na mataifa yenyewe.
Mkutano huo uliofunguliwa Jumatatu na Rais wa Zanziber, Dk. Hussein Mwinyi, ulitanguliwa na mafunzo ya siku moja ya waandishi wa habari waliopo Zanzibar kuhusu historia ya mahkama hizo, utendaji wake na matatizo yanayowakabili.
Mafunzo hayo ni sehemu ya utekelezaji wa program maalum ya kuelimisha waandishi wa habari ili kueleza umma barani Afrika umuhimu wa mahkama hizo na kuhamasika kujitokeza kwa wingi kufungua mashauri kwa vile haki yoyote ni lazima ipiganiwe. Waandishi wapatao 30 walihudhuria mafunzo hayo.
Mahkama hizo zimekuwa katika mtihani wa maamuzi yake kusita kutekelezwa na hivyo kusababisha haki za watu kudharauliwa. Mahkama ya Afrika na ile ya Afrika Mashariki zina makao yake jijini Arusha, Tanzania.
Leave a comment