JESHI la Polisi Mkoa wa Lindi nchini Tanzania, limeutawanya kwa mabomu ya machozi, mkutano wa Tundu Lissu, mgombea urais wa Tanzania kupitia Chadema aliokuwa anaufanya eneo la Somanga. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea)
Mkutano huo, umetawanywa leo Ijumaa tarehe 23 Oktoba 2020, wakati Lissu akiwa jukwaani ameanza kuwahutubia wananchi waliokuwa wamejitokeza kasikiliza.
Kabla ya kutawanya, Lissu alianza kuzungumza kwa kuwashukuru wana Somanga kwa kujitokeza ili kuwaelezea “ujumbe wa ilani ya Chadema ya uhuru, haki na maendeleo ya watu.”
Amesema, wakati wa kutafuta viongozi “ni wakati wa watu kuzungumza na kuzibana midomo.”
Lissu amesema, wamefika eneo hilo baada ya kuandika barua Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuelezea kuomba kufanya mkutano eneo hilo ambalo hakuna mgombea mwinmgine wa urais mkoani humo.
“Tumekuja hapa, lakini kuna watu wanataka kutuzuia, sisi tutazungumza, mwenye kuanzisha fujo aanzishe, mwenye kupiga watu na apige watu, ratiba ya uchaguzi na shughuli zote za mgombea urais, mamlaka inayohusika ni Tume ya Uchaguzi, si mtendaji wa kata, Rais au waziri mkuu,” alisema Lissu
Baada ya kauli hiyo, mabomu ya machozi yalifyatuliwa kuwatawanya wananchi huku Lissu mwenyewe akitulia jukwani, akiendelea kuona kinachoendelea na baadaye aliondoka jukwaani kwenda kwenye helikopita kwa ajili ya mikutano mingine mkoani humo.
Wakati akiondoka, alisikindizwa na wananchi waliokuwa wakiimba ‘rais, rais, rais…”
Leave a comment