June 26, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mkutano wa kumbana Nkurunziza waanza

Kiongozi wa Chama cha Upinzani cha Burundi, UPD-ZIGAMIBANGA, Mugwengezo Chauvineau akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam leo (hawapo pichani) kuhusu ombi lake kwa marais wa Afrika Mashariki kuepusha vurugu nchini kwao

Spread the love

MKUTANO wa Mawaziri wa Afika Mashariki (EAC), umefunguliwa leo jijini Dar es Salaam huku agenda ikiwa ni kujadili hatua zinazopaswa kuchukuliwa kesho na marais wa Jumuiya hiyo kuhusu mgogoro wa kisiasa nchini Burundi. Anaandika Pendo Omary … (endelea).

Marais hao, Uhuru Kenyetta (Kenya), Yoweri Museven (Uganda), Paul Kagame (Rwanda) na Pierre Nkurunziza, watakutana kesho jijini Dar es Salaam chini ya mwaliko wa mwenyeji wao, Jakaya Kikwete, aliye mwenyekiti wa sasa wa jumuiya hiyo.

Mkutano huo wa mawaziri umefunguliwa na Mwenyekiti wa mawaziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa EAC, Bernard Membe, ambaye pia ni Waziri wa Mambo ya Nje wa Tanzania.

Membe amesema “tutapokea mchango kutoka mwakilishi wa Umoja wa Mataifa anayeshughurikia masuala ya Ukanda wa Maziwa Makuu, wawakilishi kutoka Umoja wa Afrika na undani wa taarifa kutoka kwa Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Burundi”.

“Pia tutapokea taarifa kutoka kwa Waziri wa Afrika Mashariki wa Burundi ili kesho tuwapatie Marais njia mbadala ambazo wanaweza kuzifuata ili kutafuta ufumbuzi wa matatizo ya Burundi,” amesema Membe.

Mbali na viongozi hao, pia mawaziri hao watapata mchango wa wazee waliokuwa wakifuatilia tatizo la Burundi akiwemo Waziri Mkuu mstaafu wa Tanzania, Jaji Joseph Sinde Warioba.

Membe amesema kwa sasa Burundi inajiandaa na Uchaguzi Mkuu huku nchi hiyo ikikabiliana na matatizo ya kiusalama ambapo imesababisha wakimbizi wa nchi hiyo kufikia 50,000 katika nchi za Tanzania na Rwanda huku idadi hiyo ikiongezeka kila siku.

Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wakijadili hatua zinazopaswa kuchukuliwa na Marais wa EAC kuhusu mgogoro unaoendelea Burundi
Mawaziri wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) wakijadili hatua zinazopaswa kuchukuliwa na Marais wa EAC kuhusu mgogoro unaoendelea Burundi

“Rais Kikwete aliwatuma Mawaziri wa Mambo ya Nchi za Nje kwenda Burundi kupata taarifa za ndani na za sasa ili kumwandaa yeye na viongozi wa Afrika Mashariki kuja Dar es Salaam kesho kujadili matatizo yanayoikabili Burundi ili kupata suluhu,” amesema Membe.

Wakati huo huo, wakuu wa nchi za Afrika Mashariki, wametakiwa kutumia mbinu za kisiasa na kidiplomasia kumshawishi Rais Nkurunziza kuacha kugombea nafasi ya urais muhula wa tatu.

Akizungumza leo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Chama cha UPD –ZIGAMIBANGA, Mugwengezo Chauvineau cha nchini Burundi, amesema “mbali na kumshawishi Rais Nkurunziza kuachana na mpango wake wa kuwania nafasi hiyo katika uchaguzi ujao, pia wanapaswa kumlazimisha kuondoa silaha zilizozagaa mitaani”.

Ameongeza kuwa, “tupo hapa Tanzania kufuatilia kwa karibu kuhusu mazungumzo juu ya Rais Nkurunziza kutaka kugombea urais kwa muhula wa tatu. Marais wa Afrika Mashariki wamshauri Rais Nkurunziza na serikali yake kuandaa mazingira bora ili uchaguzi ufanyike kwa haki na huru.”

Chauvineau amefafanua kuwa, tangu kuanza kwa vuguvugu za machafuko nchini Burundi, wanasiasa hawako huru kutokana na kuwindwa na Serikali.

Mbali wakuu hao wa Afrika Mashariki kumtaka Nkurunziza kuachana na mpango wake, pia wametakiwa kuishawishi serikali yake kuwaachia huru mamia ya waandamanaji waliokamatawa.

“Tangu tuanze maandamano, raia wengi wamefugwa ili kuwatoa woga wa
kutokuandamana. Waandamanaji wamekuwa wakinyanyaswa, wanapigwa usiku na mchana. Tunataka sasa waachiwe huru,” ameongeza Chauvineau.

error: Content is protected !!