July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mkurugenzi wa Jiji awakwepa Ukawa

Spread the love

SARAH Yohana, Kaimu Mkurugenzi wa Jiji la Dar es Salaam amekwepa kukutana na Wabunge na Madiwani wa vyama vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa), anaandika Faki Sosi.

Wawakilishi hao wa wananchi walikwenda kwenye Ofisi ya Mkurugenzi wa Jiji kwa lengo la kutaka kujua tarehe ya uchaguzi wa Meya wa Jiji la Dar es Salaam ambao umekuwa ukihairishwa mara kwa mara bila sababu za msingi.

Akiwa kwenye Ofisi za Mkurugenzi wa Jiji, Mwita Waitara, Mbunge wa Jimbo la Ukonga pia Mwenyekiti wa Wabunge wa Ukawa Dar es Salaam amesema, kisheria siku za kuitisha uchaguzi wa Meya wa Jiji zimekishwa na kinachoendelea ni upuuzi.

“Utaratibu wa sheria umeshapita kwani zimeelekeza kuwa uchaguzi wa Meya ufanyike siku 90 baada ya Uchaguzi Mkuu,” amesema na kuongeza;

“Tumekuja ofisini hapa kupata tarehe rasmi ya uchaguzi na sio venginevyo, leo tumekuja kwa utaratibu wa kutaka kupangwa tarehe lakini wiki ijayo tutakuja kwa utaratibu mwengine.”

Katika msafara huo, Mwita ameongozana na wanasiasa mbalimbali wa Ukawa akiwemo Halima Mdee, Mbunge wa Kawe na Charles Kuyeko, Meya wa Halmashauri ya Ilala.

Ukawa baada ya kumsaka mkurugenzi huyo na kumkosa, Mwita alisema wamepewa taarifa na watumishi wa ofisi hiyo kwamba, Sarah amekwenda katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

“Tumeambiwa kuwa Mkurugenzi wa Jiji ameenda Ofisi za Takukuru,” amesema Mwita.

Amesema kwamba, baada ya taarifa hizo walilazimika kumtafuta kwa njia ya simu lakini hakupokea na kuwa, walimtumia ujumbe mfupi wa maneno (sms) lakini hakujibu.

Hata hivyo, zipo taarifa kwamba Sarah alipata taarifa ya ujio wa wabunge na madiwani hao kwenye ofisi yake.

Baada ya kuhakikisha kuwa, Sarah hawezi kupatikana kwa muda huo, kiongozi huyo wa Ukawa Jijini Dar es Salaam aliwaeleza wabunge na madiwani alioongozana nao watawanyike.

“Nyie endeleeni na majukumu mengine lakini mimi nitaendelea kuzungukia hapa mpaka nionane naye leo,” amesema.

Hata hivyo ameeleza kuwa, kesho kutakuwa na mkutano utakaoshirikisha wabunge, wadiwani na wanachama wa Ukawa ambao utafanyika Makao Makuu ya Chadema, Mtaa wa Ufipa katika Wilaya ya Kinondoni.

Kwenye ofisi hizo za jiji, wanachama wa Ukawa walioonesha kukerwa na kutopatikana kwa mkurugenzi huo, walikuwa wakiimba “Tunataka Uchaguzi.”

error: Content is protected !!