August 10, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mkurugenzi Mwanza anusurika kipigo

Kiomoni Kibamba, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza

Spread the love

VURUGU zimeibuka katika kikao baina ya Kiomoni Kibamba, Mkurugenzi wa Jiji la Mwanza na wafanyabiashara wanaodai kupandishiwa kwa kiwango cha kodi ilihali biashara zao haziendi vizuri, anaandika Moses Mseti.

Wafanyabiashara hao ambao walifika katika ofisi za jiji leo saa asubuhi, wakiongozwa na Hamad Nchora, mwenyekiti wao kwa lengo la kufanya mazungumzo na mkurugenzi huyo kuhusu ongezeko la kodi la vyumba vya maduka yao.

Wafanyabiashara hao hufanya kazi zao Soko kuu, Makoroboi na Sahara waliingia katika ukumbi wa jiji kwa ajili ya mazungumzo kufuatia bei ya pango ya sasa ni Sh. 200,000/= kwa maduka ya ndani na 250,000/= kwa maduka ya nje. Mazungumzo ambayo yalitawaliwa na mabishano makali.

Wafanyabiashara hao walidai kwamba bei inayoelekezwa na mkurugenzi huyo ya Sh. 300,000/= maduka ya ndani na Sh. 417,000/= kwa maduka ya nje katika soko hilo si halali kwani biashara kwa sasa sio nzuri.

Walidai mikataba yao inatarajiwa kuisha Julai 2017 lakini mkurugenzi wa jiji hilo ameisimamisha kwa madai kuwa faida wanayoipata wafanyabiashara hao ni kubwa ikilinganishwa na fedha inapelekwa jiji.

Msimamo huo wa mkurugenzi dhidi ya wafanyabiashara uliibua vurugu hizo zilizodumu kwa zaidi ya dakika 10 huku wengi wakitoka nje kwa hasira huku wakitupia maneno makali na kumnyooshea kidole Kibamba.

“Kesho utatuona airport (uwanja wa ndege Mwanza), wewe mkurugenzi unafanya siasa na maisha ya watu,” walifoka kwa hasira wafanyabiashara hao.

Kibamba aliwasihi wafanyabiashara hao kutulia na kurudi ndani ya ukumbi ili majadiliano yaendelee ambapo baadhi walikubali kurudi na mkurugenzi huyo kuwaangukia akisema;

“Nendeni mkaedelee na biashara zenu mpaka Julai 2017 lakini muda huo ukifika bei iliopangwa itabaki kama ilivyo, Mkaguzi wa Hesabu za Serikali alifanya uchunguzi na kubaini sisi tunapoteza fedha nyingi kwenye maduka yetu ya Soko kuu na Sahara hivyo lazima tudhibiti upotevu huo wa mapato.”

Hamad Nchora, mwenyekiti wa wafanyabiashara hao amesema hatua zilizochukuliwa na mkurugenzi huyo kuwaacha waendelee mpaka Julai mwakani ni nzuri na wafanyabiashara wameridhia na kwamba muda huo ukifika watakaa na kuangalia kufanya.

error: Content is protected !!