May 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mkurugenzi Jiji la Dar, ahamishiwa Kinondoni

Sipora Liana kuwa, mkurugenzi mpya wa Manispaa ya Kinondoni

Spread the love

 

RAIS wa Tanzania, John Magufuli amempangia kazi, Sipora Liana kuwa, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, Dar es Salaam kuanzia leo Alhamisi, tarehe 25 Februari 2021. Anaripoti Regina Mkonde…(endelea)

Sipora anakwenda kuchukua nafasi ya Aron Kagurumjuli, ambaye Rais Magufuli, alitengua uteuzi wake, tarehe 16 Februari 2021.

Rais Magufuli, amemteua Sipora siku moja baada ya kulivunja Jiji la Dar es Salaam na kuipandisha hadhi Halmashuri ya Ilala kuwa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam, huku akieleza kwamba, watumishi wa Jiji la Dar es Salaam, lililovunjwa watapangiwa vituo vingine vya kazi.

Sipora alikuwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaa, lililovunjwa.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais-Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Selemani Jafo amesema, utaratibu wa kuwahamisha wafanyakazi katika vituo vingine utaendelea.

Aidha Waziri Jafo amemkabidhi Meya wa Jiji la Dar es Salaam,Omary Kumbilamoto, gari lililokua likitumiwa na Meya wa Jiji lililovunjwa la Dar es Salaam.

Omary Kumbilamoto, Meya wa jiji la Dar es Salaam

Kumbilamoto, alikuwa Meya wa Manispaa ya Ilala iliyopandishwa hadhi kuwa Halmashuri ya Jiji la Dar es Salaam.

“Kama ilivyoelekezwa na Rais, watumishi watakuwa wanahamishiwa katika vituo vyao vya kazi. Katibu Mkuu Tamisemi nawaelekeza mfanye haraka kuwapangia vituo vya kazi,” amesema Jafo

“Gari alilokuwa anatumia Mstahiki Meya wa Jiji la awali likabidhiwe kwa Meya wa jiji jipya la Manispaa ya Ilala,” ameagiza Jafo.

error: Content is protected !!