April 11, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mkurugenzi amgomea Waziri Mkuu

Spread the love

AGIZO la Waziri Mkuu Majaliwa Kassim, kuwataka watendaji wa Serikali kutoa taarifa katika vyombo vya habari juu ya mipango ya maendeleo inayofanywa na serikali, limepuuzwa na Godwin Kunambi, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya Dodoma, anaandika Dany Tibason.

Leo baada ya kumalizika kwa zoezi la usafi uliofanyika ili kuadhimisha siku ya kumbukumbu ya Mwalimu Julius Nyerere, muasisi wa Taifa la Tanzania, Kunambi amekataa kuzungumzia lolote juu ya utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu la kuondoa nyumba za tope katikati ya Mji wa Dodoma.

“Siwezi kuongea jambo lolote kwa sasa ninawaachia Mkuu wa Wilaya na Mkuu wa Mkoa waongee. Bora ningekuwa nazungumza na radio au TV lakini katika gazeti siwezi kuzungumza chochote, niache tu,” amesema Kunambi alipozungumza na mwandishi wa MwanaHALISI online. 

Pamoja na mwandishi kumkumbusha kuwa Mkurugenzi ndiye mtendaji mkuu wa manispaa hivyo ni vyema akatoa ufafanuzi juu ya hatua gani ambazo manispaa yake imezichukua mpaka sasa ili kutekeleza agizo la Waziri Mkuu la kuondoa nyumba za tope na kuboresha miundombinu lakini Kunambi aligoma.

Hivi karibuni baada ya kuanza utekelezaji wa kuifanya Dodoma kuwa makao makuu ya nchi, Waziri Mkuu Majaliwa alijitambulisha kwa waandishi wa habari wa Mkoa wa Dodoma na kuwaagiza wakuu wa Idara mbalimbali pamoja na watendaji wa serikali kuhakikisha wanatoa ushirikiano kwa vyombo vya habari.

“Toeni taarifa za utekelezaji wa mipango ya maendeleo ya serikali katika vyombo vya habari bila kukibagua chombo chochote,” alisema Waziri Mkuu Majaliwa.

Kitendo cha Kunambi kukataa kuzungumzia mipango ya maendeleo hususani utekelezaji wa agizo la Waziri Mkuu la kuondoa nyumba za tope katikati ya mji ni kupuuza agizo lake la awali la kutaka taarifa muhimu za mipango ya maendeleo zitolewa katika vyombo vya habari bila kuvibagua vyombo hivyo.

error: Content is protected !!