June 27, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mkurugenzi ahamishwa kwa kukataa ‘bao la mkono’

Spread the love

MKURUGENZI wa Jiji la Mwanza, Hassan Hida, anadaiwa kuhamishwa katika jiji hilo kwa kile kinachodaiwa ni kukataa kucheza ‘bao la mkono’ katika Jimbo la Nyamagana. Anaandika Moses Mseti, Mwanza … (endelea).

Inadaiwa kuwa mkurugenzi huyo ameondolewa katika jiji hilo baada ya kukataa kucheza ‘bao la mkono’, huku akituhumiwa kumuunga mkono Mgombea Urais wa Chadema, Edward Lowassa anayeungwa mkono na Muungano wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Inaelezwa kuwa Hida kabla ya kuondolewa katika nafasi hiyo na kupewa kazi nyingine serikalini, baadhi ya viongozi wakubwa wa mkoa huo, waliitisha vikao vya kumlazimisha kucheza ‘bao la mkono’ jambo ambalo alipingana nalo na kibarua chake kuota mbawa.

Hata hivyo baada ya mkurugenzi huyo kukataa mchezo huo hatari, viongozi hao wa juu walianza kuwasiliana na viongozi wa kitaifa wakiomba kuondolewa kwake jambo ambalo halikuchukua muda mrefu na kuhamishwa.

Mtoa taarifa hizi amesema kuwa mkurugenzi huyo, aliondolewa kutokana na kuwagomea viongozi hao wanaodaiwa kuunda mbinu chafu za kulazimisha ushindi katika Jimbo hilo la Nyamagana ambalo historia ya wabunge waliowahi kuongoza wamekaa kwa awamu moja.

Mtoa taarifa aliendelea kudai kuwa Chama cha Mapinduzi (CCM) kimejipanga kulazimisha ushindi wowote ule hata kama ni wa kumwaga damu lakini washinde jimbo hilo kitendo ambacho kitasababisha uvunjifu wa amani.

“CCM wameisha jiapiza kwamba jimbo hili na lile la Ilemela ni lazima washinde hata kama ni wa kumwaga damu na huyu mkurugenzi kahamishwa kwa sababu aliwakatalia kutangaza matokeo ya uongo,” amesema mtoa taarifa huyo.

Hata hivyo Hida ambaye alishawahi kuwa Mkurugenzi wa Jiji la Arusha, kabla ya Mwanza na kuhamishwa katika nafasi hiyo, inadaiwa kuwa na msuguano na Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Magesa Mulongo, ambao wote walihamishiwa Mwanza kutoka Arusha.

Hata hivyo Hida alipotafutwa na gazeti hili kuzungumzia tuhuma za kuondolewa kwake jijini hapa zinazohusishwa na siasa, simu yake ya mkononi haikupatikana.

Jimbo la Nyamagana linashindaniwa na Ezekia Wenje (Chadema), anaetetea nafasi hiyo, Stanslaus Mabula (CCM) na wagombea wengine wa ACT, TLP.

error: Content is protected !!