May 21, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mkude atozwa faini milioni 2, aitwa kambini

Spread the love

 

KAMATI Nidhamu ya Klabu ya Simba ya Dar es Salaam, imemkuta na hatia kiungo wa klabu hiyo, Jonas Mkude ya utovu wa nidhamu na kumhukumu kulipa Sh.2 milioni. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam … (endelea).

Pia, kamati hiyo, imemtaka Mkude kuripoti kambini haraka ili kuendelea na majukumu ya kuwatumikia mabingwa hao watetezi wa ligi kuu ya vodacom Tanzania Bara.

Hukumu hiyo, ilitolewa jana jioni Jumamosi tarehe 23 Januari 2021 na Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Suleiman Kova, baada ya kukutana na Mkude ambaye aliwasilisha utetezi wake, katika makosa makosa matatu.

Mkude alisimamishwa na uongozi wa Simba, tarehe 28 Desemba 2020 pamoja na mambo mengine “tuhuma za utovu wa nidhamu zinazomkabili.”

Kova amesema, kosa la kwanza ni kutohudhuria semina elekezi iliyohusisha wachezaji, benchi la ufundi na viongozi iliyofanyika Septemba 2020 jijini Dar es Salaam.

Amesema, Mkude amekiri kosa hilo na adhabu yake ni faini ya Sh.1 milioni.

Katika kosa la pili, Kova amesema, Mkude alichelewa kuingia kambini wakati timu ilipokuwa ikijiandaa na mchezo dhidi ya Coastal Union.

Amesema, kosa kama hilo, amekuwa akilifanya mara kwa mara “hiyo amepewa adhabu ya karipio kali na faini ya Sh.1 milioni pamoja na kuwekwa kipindi cha uangalizi cha miezi sita. Kama atarudia kosa hili, basi atashtakiwa na anaweza kukutaka na adhabu kali ikiwemo hata kufukuzwa kwenye timu.”

Kova aliyewahi kuwa Kamanda wa Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam amesema, kosa la tatu, ni kutoripoti kambini siku ya tarehe 26 Desemba 2020 bila ruhusa.

Amesema, katika tuhuma hiyo, kamati haikumkuta na hatia baada ya kamati kutothibitisha pasipo shaka shitaka hilo kwani sekretrieti iliyowasilisha mashtaka ilishindwa kuthibitisha.

Baada ya kumaliza kutoa hukumu hiyo, Kova alitoa maagizo ya kamati ya kumtaka Mkude “kurejea kambini mara moja kuendelea na mazoezi na asipofanya hivyo atakuwa amefanya tena kosa la utovu wa nidhamu na pia, anapaswa kuomba radhi kwa maandishi ndani ya saa 24 tangu hukumu hii ilipotoka.”

Hukumu ilitoka jana Jumamosi saa 11 jioni huku faini akitakiwa kuilipa ndani ya mwezi mmoja.

error: Content is protected !!