KIUNGO wa klabu ya Simba, Jonas Mkude amerejea kambIni mara baada ya sakata lake kumalizika ndani ya klabu hiyo baada ya kutakiwa kuomba msamaha na kulipa faini ya Sh. 2,000,000 kama ilivyoeleza kamati ya nidhamu ya klabu hiyo. Anaripoti Kelvin Mwaipungu, Dar es Salaam … (endelea).
Tarehe 28 Desemba 2020, uongozi wa klabu ya Simba ulimsimamisha mchezaji huyo kutokana na makosa ya utovu wa nidhamu na kesi yake ikaenda kusikilizwa kwenye kamati ya nidhamu iliyopo chini ya Seleman Kova.
Taarifa ya kurejea kwake kambini iliripotiwa jana kupitia ukurasa wa klabu ya Simba uliopo kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram kwa kuweka picha ya mchezaji huyo akiwa anafanya mazoezi binafsi.
Licha ya kurejea kwake kambini kiungo huyo ameachwa kwenye listi ya wachezaji waliosafiri kuelekea Dodoma kwenye mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara dhidi ya Dodoma Jiji utakaochezwa kesho tarehe 4 Februari 2021.
Ikumbukwe mara baada ya kusimamishwa mchezaji huyo aliomba radhi tarehe 21 Januari 2021, na kutaka wanachama, uongozi na mashabiki wa klabu hiyo kumsamehe kwa kosa alilofanya ili aweze kurejea mazoezini.
Leave a comment