January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mkotya ambana mbavu Nkamia

Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Juma Nkamia akiwa moja ya shughuli za kisiasa jimboni kwake

Spread the love

MHARIRI wa Gazeti la Mtanzania, Khamis Mkotya ni miongoni mwa makada saba wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), wanaotajwa kumnyima usingizi mbunge wa sasa wa Chemba (Kondoa Kusini), Juma Nkamia-aliye Naibu Waziri wa Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo. Anaandika Mwadishi Wetu … (endelea).

Mkotya ambaye bado hajatangaza nia rasmi, jina lake limevuma kwa kiasi kikubwa jimboni humo na kuzusha hofu kwa Nkamia ambaye anadaiwa kumjengea chuki.

“Nyota ya Mkotya inamnyima sana usingizi Nkamia, yaani amefikia mahali hata tunapokuwa kwenye shughuli za kuripoti vikao vya Bunge mjini Dodoma… Nkamia akipisha na Mkotya akisalimiwa haitikii.

“Kinachomkera ni kuona namna Mkotya anavyoungwa mkono na wananchi wa jimbo hilo hadi kufikia wakati wa kumpigia simu au kumwita kumweleza kero zao wakati akiwa bado sio mbunge,”anasema mmoja wa wahariri.

Mbali na Mkotya, wengine wanaotajwa ni Raphael Kilesa, ambaye ni Ofisa Utamaduni wa Wilaya, Juliana Maghembe- mtumishi wa benki moja jijini Dar es Salaam, Fred Duma, Said Sambala ambaye ni Diwani wa Kata ya Mondo na wengine.

Jimbo hilo lenye tarafa nne za Goima, Mondo, Kwamtoro na Farkwa ni kati ya majimbo yanayokabiliwa na changamoto nyingi ikiwamo uhaba wa huduma za kijamii kama vile maji, afya, elimu, miundombinu na migogoro ya ardhi.

Chemba ni moja ya majimbo tisa yaliyopo Mkoa wa Dodoma ambayo yanaonekana kuwa ngome ya CCM, kutokana na chama hicho kuungwa mkono zaidi kuliko vyama vya upinzani.

Hata hivyo, Nkamia kupitia kwa marafiki zake wa karibu amekuwa akikiri kuwa Mkotya anamsumbua na kwamba hana hofu na wagombea wengine.

Kwa mujibu wa watu hao, Nkamia hana hofu na wagombea hao kwani walio wengi alishindana nao katika uchaguzi wa 2010 akawashinda, hivyo anajua udhaifu wao.

Mbunge wa zamani aliyeangushwa 2010, Pascal Degera naye anatajwa kurudi ulingoni. Mgombea huyo hana madhara kwani licha ya umri wake kuwa mkubwa lakini amekuwa mbunge wa jimbo hilo kwa vipindi vinne mfululizo (miaka 20), hivyo anaonekana hana jipya.

Upepo wa kisiasa kwa Nkamia unamvumia vibaya, kwani jimboni kwake malalamiko ya wananchi ni mengi dhidi yake.

Moja ya vitu vinavyomtafuna Nkamia ni ahadi alizotoa wakati wa kampeni za mwaka 2010. Anadaiwa kuwa na ahadi nyingi ambazo ameshindwa kuzitekeleza.

Mbali ya ahadi, suala la tabia na kauli za kukarahisha wapigakura wake ni miongoni mwa vitu vinavyomuweka katika wakati mgumu.

Uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Desemba mwaka jana, ni moja ya kielelezo kilichodhihirisha kuwa mbunge huyo amechuja, baada ya vyama vya siasa vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) kuzoa vijiji vingi wilayani Chemba.

Katika uchaguzi huo, vyama vya upinzani vimechukua vijiji 27 na vitongoji zaidi ya 102 katika jimbo hilo kutoka vijiji 12 walivyokuwa navyo hapo awali.

Wakati wa kampeni za uchaguzi huo, Nkamia kama mbunge wa jimbo alishiriki kupanda majukwaani kuwanadai wagombea wa CCM, lakini jambo la kushangaza katika vijiji vyote alivyokwenda CCM imeshindwa.

Nkamia mbali ya kuwa mbunge na naibu waziri, vile vile ni Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC) na Kamanda wa Vijana wa Wilaya.

error: Content is protected !!