January 19, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mkono kufilisi nchi

Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono

Mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono

Spread the love

KAMPUNI ya mbunge wa Musoma Vijijini (CCM), Nimrod Mkono inadaiwa kulipwa na TANESCO, takriban shilingi 18 bilioni kwa huduma ya ushauri, MwanaHalisi Online limegundua.

Nyaraka ambazo gazeti hili limeona zinaonyesha kuwa tayari kampuni ya Mkono imetumia kiasi hicho kutoka shirika la umeme linalolegalega kifedha.

Mkono na kampuni yake ya Mkono & Co. Advocates ya jijini Dar es Salaam, amekuwa mshauri wa kisheria na wakili wa TANESCO tangu Mei 1995.

Nyaraka zinaonyesha kuwa shilingi 18 bilioni zimelipwa kwa ushauri na utetezi ambao kampuni ya Mkono imefanya katika minyukano ya kudaiana kati ya TANESCO na kampuni nyingine ya umeme, Independent Power Tanzania Limited (IPTL).

Hivi sasa uhusiano wa TANESCO, kampuni ya umeme ya serikali na kampuni ya Mkono, umekuwa wa kilio kama mawasiliano ya ndani yanavyoonyesha.

Moja ya mawasiliano hayo ni barura ya Jenerali Robert Mboma, mwenyekiti wa bodi ya wakurugenzi TANESCO, ambayo inalalamikia matumizi ya mabilioni ya shilingi ya kampuni ya Mkono, tena bila mafanikio.

Barua ya Mboma ya 10 Septemba 2013; kwenda kwa Mkono, inalalamikia matumizi ya kiasi hicho cha fedha katika mashauri ambayo yamechukua muda mrefu na bila kuleta tija.

Barua yenye Kumb. Na. SEC.427/IPTL/9/2013; ambayo imebeba kichwa cha maneno kisemacho, “Ushauri ambao kampuni yako imetoa kwa Tanzania Electric Supply Company Limited,” imenukuliwa kwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo.

“Kwa sasa, kulingana na kumbukumbu tulizonazo, kampuni yako imekwishatumia takribani Sh. 18 bilioni kama gharama za ushauri katika kusimamia suala hili kufikia Aprili 2013,” anaeleza Jenerali Mboma.

Anasema, “Hiki ni kiasi kikubwa mno cha fedha za walipa kodi ambazo zingeweza kuwekezwa kwenye miradi mingine ya uzalishaji kwa manufaa ya Watanzania wote.”

Kana kwamba hiyo haitoshi, Mboma anasema, “TANESCO inataka ieleweke kuwa inasikitishwa na namna kampuni yako ilivyotoa ushauri wa kisheria kuhusiana na mivutano iliyohusu Mkataba wa mauziano (PPA) wa tarehe 26 Mei 1995 kati yetu na IPTL, kwa vile ulivyotushauri na katika kuisimamia kesi tangu ilipofunguliwa mwaka 1998.”

TANESCO sasa inatuhumu kampuni ya mkono kutoishauri vizuri hadi kupoteza kesi yake dhidi ya IPTL.  Kesi ambayo TANESCO inasema imeipoteza kwa kutoshauriwa vizuri inahusu mkataba wa kununua umeme – Power Purchase Agreement (PPA) wa 26 Mei 1995.

Kampuni ya IPTL ndiyo kampuni ya kwanza ya nje kuingiza mitambo ya kuzalisha umeme wa dharula nchini. Mitambo yake inatumia mafuta mazito (Industrial Diezel Oil – IDO); jambo ambalo linasababisha umeme inaozalisha kuwa ghali kuliko ule wa kuzalisha kwa kutumia gesi na, au maji.

Taarifa kutoka ndani ya TANESCO zinasema, mbali na malipo kwa Mkono, kampuni ya IPTL hukomba kiasi cha Sh. 1.8 bilioni kila mwezi zikiwa malipo kwa gharama za kuweka mitambo yake nchini – Capacity Charge.

Mtoa taarifa kutoka ndani ya serikali anasema, kwa kuwa TANESCO inakabiliwa na ukata mkubwa wa fedha kutokana na mikataba ya kinyonyaji ya umeme, serikali hutoa kila mwezi, kiasi cha Sh. 3.8 bilioni kuwezesha shirika hilo kununua mafuta ya kuendesha mitambo ya dharula.

(Waziri, Katibu mkuu, Mboma, Mkono, TANESCO na CEO wanasemaje?)

Kampuni ya Mkono imo katika umoja na kampuni ya SNR Denton. Imeelezwa kuwa umoja huo wa kampuni unaundwa na zaidi ya wanasheria 1,100 wa Uingereza, Marekani, Canada na Tanzania; na una makao makuu jijini London, Uingereza.

TANESCO limeeleza kwamba lilishauriwa na wanasheria wa Mkono & Co. Advocates kuwa lina hoja za msingi kudai urekebishaji wa kiwango cha bei na kwamba “TANESCO watapaswa kudai kiasi kitakachokuwa kimezidi kutokana na ankara za IPTL zilizotozwa baada ya maamuzi.”

“…ulitushauri tutoe indhari ya madai ya ankara za ziada kwa IPTL. Tukapinga ankara za malipo zilizohusu gharama za kuweka mitambo – Capacity Charge. Yote haya yalifanywa kwa kuzingatia ushauri wako,” imeeleza barua ya Mboma kwa Mkono na kwamba hatua hiyo haikufanikiwa.

Katika barua , TANESCO inalalamikia kampuni ya Mkono kwamba pamoja na kutoa ushauri 30 Juni 2004 kuwa shirika hilo lina hoja za msingi na halali kuomba urekebishaji wa bei ya umeme na kurudishiwa malipo ya ziada, lakini 4 Oktoba 2012, Mkono alikwenda na mtizamo tofauti.

“Katika barua yako ya 4 Oktoba 2012, umesema kuna uwezekano mdogo sana wa kushinda kesi hiyo kutokana na kugundulika kwa baadhi ya nyaraka zilizodhoofisha utetezi uliotolewa mapema na shirika,” barua ya Mboma inaeleza.

Inaongeza, “Ulitushauri kwa hoja nzito kuwa tupiganie usuluhishi na Benki ya Hong Kong – SCB HK au kampuni yako ielekezwe zaidi kuwasilisha ombi la kukataliwa kwa uamuzi unaoinufaisha benki hiyo,” Mboma anaeleza Mkono kwa njia ya malalamiko.

Barua ya shirika hilo inajibu maelezo ya Mkono ya kutaka malipo ya ziada ya fedha kwenye kesi hiyo wakati TANESCO haioni manufaa ya malipo hayo.

Wakati wote wa mgogoro, fedha zilizokuwa zinabishaniwa mahakamani, ziliingizwa kwenye akaunti maalum iliyofunguliwa Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Kutokana na mfumo huo wa kubishania ankara, IPTL ilifungua malalamiko mbele ya Taasisi ya Usuluhishi wa Migogoro ya Uwekezaji (ICSID) wakitaka kupatikana tafsiri halisi ya eneo hilo kulingana na mkataba wa mauziano ya umeme.

Katika hatua hiyo, TANESCO inalalamikia kampuni ya Mkono ambayo iliiwakilisha mpaka pale shauri hilo lilipofutwa kwa  manufaa ya IPTL kutokana na amri iliyotolewa 19 Agosti 2010.

Kwa barua ya kampuni ya Mkono ya 4 Oktoba 2010, TANESCO inajulishwa kuhusu nia ya benki ya Standard Chartered Hong Kong (SCB HK) kufungua ombi la usuluhishi baada ya IPTL kuacha kuendelea kwa shauri.

Matokeo yake, mbali ya kuihakikishia TANESCO kuwa itashinda, ikashauri pia shirika lielekeze kampuni hiyo ya uwakili kuendelea kutaka kusimamishwa kwa usajili wa malalamiko ya SCB HK mbele ya ICSID kwa hoja kwamba SCB HK haina uhalali katika suala hilo. TANESCO walitoa maelekezo hayo kwa mawakili wa Mkono.

Hata hivyo, TANESCO inalalamika kuwa mawakili hao walishindwa kuzuia SCB HK kusajili malalamiko yake na hatimaye, “Ombi (letu) kuhusu suala hilo lilitupwa.”

“Usajili wa SCB HK ulikubaliwa na ICSID, na ukasikilizwa kama ulivyopangwa,” imesema TANESCO katika barua yake kwa kampuni ya Mkono.

Mara tu usikilizaji wa usuluhishi ulipofungwa Aprili 2013, TANESCO inasema kampuni ya uwakili ya Mkono ilishauri shirika kufungua ombi la kucheleweshwa tamko la ICSID la kuipa SCB HK ushindi mpaka kwanza kusubiri uamuzi wa ombi la SCB HK lililokuwa likiendelea kusikilizwa kwenye Mahakama Kuu ya Tanzania.

“TANESCO ilizuia, lakini pia ilishindwa. ICSID ilisema kuwa itatoa tamko lake ndani ya miezi mitatu,” barua ya Mbona inaeleza.

TANESCO, mbali na kulipa mabilioni hayo ya shilingi kwa ushauri, imekuwa ikilipa fedha nyingi kwa makampuni yanayodai kutoa huduma za kisheria, ikiwamo kesi kati ya shirika hilo na makampuni ya Richmond Development Company (DRC), Dowans Holding na Dowans Tanzania Limited.

Kuibuka kwa taarifa hizi kumekuja miaka sita baada ya Mkono kutajwa na kiongozi mkuu wa upinzani nchini, Dk. Willibrod Slaa kuwa ni miongoni mwa watuhumiwa 11 wa ufisadi nchini.

Mbele ya umati mkubwa, kwenye mkutano wa hadhara katika viwanja vya Mwembeyanga, Temeke, Dar es Salaam, Dk. Slaa alisema Mkono, kupitia kampuni yake ya Mkono & Co. Advocates amekuwa akilipwa malipo makubwa, hasa yale yanayohusu kesi ya Valambhia, ambamo BoT inadaiwa jumla ya Sh. 60 bilioni.

Dk. Slaa alisema, kwa mujibu wa Mkaguzi na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), kampuni ya Mkono tayari imelipwa zaidi ya Sh. 8.1 bilioni, fedha taslimu kwa kesi hiyo ambayo bado iko mahakamani. Malipo hayo, wakati huo, yalikuwa sawa na asilimia 13.5 ya deni lote inalodaiwa BoT.

Chini ya Kanuni za Malipo ya Mawakili na Uamuzi wa Gharama za Kesi za mwaka 1991 (Tangazo la Serikali Na. 515 la 1995), kiwango cha malipo ya mawakili katika kesi ambazo fedha inayodaiwa ni zaidi ya Sh. 10 milioni, kitakuwa asilimia tatu.

Kwa kufuata masharti ya sheria hii, kampuni ya Mkono ilipaswa kulipwa Sh. 1.8 bilioni.

Aidha, kampuni ya Mkono inatajwa katika taarifa ya uchunguzi kuhusu tuhuma dhidi ya makampuni ya Tanfarms Ltd., Makinyumbi Estates Ltd., Centrepoint Investments Ltd., na Arusha Farms Ltd., yanayomilikiwa na V. G. Chavda kuhusiana na matumizi mabaya ya fedha za Debt Conversion Programme.

error: Content is protected !!