Friday , 3 February 2023
Home Gazeti Habari Mke wa Sabaya apanda kizimbani kumtetea mme wake
Habari

Mke wa Sabaya apanda kizimbani kumtetea mme wake

Lengai ole Sabaya
Spread the love

 

MKE wa mfungwa, Lengai ole Sabaya, aitwaye Jesca Nassari (28) ameieleza Mahakama kuwa namba ya simu 0758707171 inayodaiwa kuwa ya Sabaya, amekuwa akiitumia kwenye shughuli zake za ujasiriamali. Anaripoti Mwandishi Wetu…(endelea).

Aidha, amedai tangu wafunge ndoa mwaka 2018 wamekuwa wakimiliki pamoja biashara za mahindi na maharage, waliyoanza kwa mtaji wa Sh.3 milioni na sasa hajui wana kiasi gani cha fedha kupitia biashara hiyo, ambayo wanauza magunia kati ya 200 na 300.

Pia, amesema hawajasajili jina la biashara na hawana leseni na hawalipi kodi, kutokana na biashara hizo, kwani hulipia ushuru sokoni na mnadani wanapouza mifugo kwa alichoeleza kuwa ni ujasiriamali.

Jesca alisema hayo kwa nyakati tofauti jana Jumatatu, tarehe 17 Januari 2022, mbele ya Hakimu Mkazi, Patricia Kisinda akiongozwa kutoa ushahidi na Wakili wa Sabaya, Moses Mahuna na kuulizwa maswali ya dodoso na Wakili wa Serikali Mwandamizi, Ofmed Mtenga.

Alieleza mahakamani hapo, kuwa tarehe 22 Januari 2022 asubuhi, alipigiwa simu na dalali wa mazao na saa tano akaelekea Arusha kukutanishwa na mnunuzi wa maharage, ambapo alikwenda eneo la Kisongo ilipo stoo yake ya mazao.

Hata hivyo, alidai mahakamani hapo kutomfahamu kwa sura wala jina dalali aliyekuwa akiwasiliana naye, kwani hakuwahi kuonana naye uso kwa uso.

Jesca aliiambia Mahakama kuwa ndiye anasimamia biashara hizo na wana kuku 600 huku akidai kuwa hajui idadi ya ng’ombe wala mbuzi wanaomiliki.

Sehemu ya mahojiano baina ya Jesca na Wakili yalikuwa kama ifuatavyo:

Wakili: Januari 22 mwaka jana ulikuwa wapi?
Shahidi: Nakumbuka nilikuwa Bomang’ombe, Hai, Kilimanjaro.

Wakili: Kule Bomang’ombe ulikuwa unafanya nini?

Shahidi: Nilikuwa ofisini kwa Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Hai.

Wakili: Ulikuwa unafanya nini?

Shahidi: Nilikuwa najitolea kwenye Idara ya Kilimo na Umwagiliaji.

Wakili: Ulikuwa unajitolea kama nani?

Shahidi: Irrigation engineer.

Wakili: Ikumbushe Mahakama, siku hiyo ulifanya kazi hadi saa ngapi?

Shahidi: Nilikuwapo kuanzia saa mbili asubuhi hadi saa 9:30 kuelekea saa 10 jioni.

Wakili: Na baada ya saa 10 ulielekea wapi?
Shahidi: Nilielekea nyumbani nilipokuwa naishi kupumzika.

Wakili: Alikuja shahidi wa Jamhuri namba 13 akieleza Mahakama Januari 22 mwaka jana, ukiambatana na watu wengine mlikwenda gereji ya Mroso una kipi cha kuiambia Mahakama?

Shahidi: Shahidi huyo ni wa uongo, alikuja kutoa ushahidi wa uongo dhidi yangu, kwani sikuwahi kufika gareji ya Mroso na wala hiyo gereji siifahamu na hata Mroso mwenyewe simfahamu. Na vile vile Mheshimiwa hakuna shahidi aliyeletwa na upande wa mashitaka, aliyekuja kusema hiyo siku nilikuwapo na si Mroso, mlinzi wala karani wake.

Kama ni kweli nilikuwapo siku hiyo, hao watu wangeniona. Na vile vile shahidi namba 13 alipata taarifa fiche, kwamba nilikuwa kwenye gari, Wangemleta dereva wangethibitisha kama kweli nilikuwapo.

Wakili: Shahidi yule alisema kuna watu ulikuwa nao na walikiri ulikuwapo, una kitu gani cha kuiambia Mahakama?

Shahidi: Hao watu siwafahamu, ni watu niliowafahamia hapa mahakamani na kama ni kweli, angeleta maelezo ya hao watu anaosema walikiri ili kuthibitisha aliyosema.

Wakili: Shahidi wa Jamhuri namba 13 aliimbia Mahakama kuwa Januari 22 mwaka huu ulipata mgao wa Sh milioni 2.4 sehemu inayoitwa Tulia kutoka kwa Sabaya, una kitu gani cha kuiambia Mahakama?

Shahidi: Shahidi huyo ni mwongo; kwani mimi binafsi siku hiyo sikuwahi kufika Tulia Hotel kwa muda huo aliosema shahidi, na wala kupokea kiasi hicho cha fedha kutoka kwa Sabaya.

Vilevile nilisikia Tulia ni hoteli, nadhani ina mmiliki, meneja na wahudumu, na kama nilikuwapo angekuja mhudumu aliyetuhudumia siku hiyo na kutoa ushahidi wake hapa mahakamani.

Alidai hela ziligawiwa chumbani, ambako mimi nilikuwa nagawiwa na yule mtu anayetoa, angemhoji mtu aliyedai kutoa hizo pesa, ambapo alikiri hapa hakuwahi kumhoji huyo mtu au angalau kama ofisa uchunguzi angenihoji, ila alikiri hapa hakuwahi kunihoji.
Kwa hiyo shahidi ni mwongo aliyetunga maneno na aliyejipanga kuja kuongea uongo mbele ya Mahakama yako.

Wakili: Shahidi huyo wa 13 alisema kuna watu ambao mlikuwa nao na ndiyo waliomthibitishia kuhusu mgao huo, una kitu gani cha kuiambia Mahakama kuhusu suala hilo?

Shahidi: Mheshimiwa Hakimu, shahidi huyo ni mwongo, na hao watu aliosema siwafahamu kabla, ni watu ambao nimekuja kuwafahamu baada ya kufunguliwa kesi.

Kama ni kweli, aliandika maelezo na wamenitaja angeleta hayo maelezo hapa mahakamani, ili kusiwe na shaka yoyote ni kweli aliwahoji na kusema nilikuwapo.

Wakili: Shahidi alikuja shahidi wa 13 wa Jamhuri, akasema Januari 22 mwaka jana, wewe na watuhumiwa wengine mlikaa Point Zone kupanga uhalifu, una kitu gani cha kuiambia Mahakama?

Shahidi: Mheshimiwa, shahidi huyo ni mwongo. Na mimi sikufika Point Zone siku hiyo kama alivyodai, naamini ni sehemu ya hoteli, kuna watu na wahudumu, meneja nadhani angeleta mmoja wa hao watu aliosema nilikuwa nao Point Zone ili kuthibitisha kweli nilikuwa hapo.

Wakili: Shahidi huyo alisema kuna watu ulikuwa nao na walimthibitishia ulikuwa Point Zone?

Shahidi: Shahidi huyo ni muongo na watu hao siwafahamu na kama ni kweli walimthibitishia, angeleta hayo maelezo hapa mahakamani.

Wakili: Alikuja shahidi namba 12 akasema Februari 2 mwaka jana, ulikuwa Blackhood Apartment, Dar es Salaam, ukiwa na watu wengine, una kitu gani cha kuiambia Mahakama?

Shahidi: Shahidi huyo ni muongo na mimi sikuwa kwenye hizo Apartments siku hiyo na kama ningekuwapo na kulikuwa kuna biashara aliyokuwa anafanya, ningeshiriki au ningekuwa shahidi katika hiyo biashara.

Wakili: Iambie Mahakama ulikamatwa lini na wapi?

Shahidi: Mei 28 mwaka huu, niliitwa ofisi za Takukuru Upanga, wakisema wanataka kunihoji na nilikamatwa kuanzia siku hiyo, hadi nafikishwa mahakamani.

Wakili: Hebu iambie Mahakama kuanzia 22.1.2021 hadi 27.5.2021 ulikuwa wapi?

Shahidi: Nakumbuka nilikuwa kati ya mikoa ya Kilimanjaro na Dar es Salaam.

Wakili: Wakati unakamatwa, walikwambia unatuhumiwa kwa kosa gani?

Shahidi: Sikuambiwa nakamatwa kwa kosa gani na sikuhojiwa kwa kosa lolote.

Wakili: Ulipofikishwa ofisi za Takukuru ni nani alikuchukua maelezo ya onyo?

Shahidi: Hakuna aliyenichukua maelezo ya onyo wala kunihoji.
Wakili: Iambie Mahakama ulikaa rumande siku ngapi kabla ya kupelekwa mahakamani?
Shahidi: Siku 8.

Leave a comment

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Related Articles

HabariHabari Mchanganyiko

CRB yashtukia makandarasi wanaofanya ubia wa ujanja ujanja, yasema watakaobainika kuchukuliwa hatua kali

Spread the love  BODI ya Usajili wa Makandarasi (CRB), imeonya makandarasi wanaofanya...

HabariKimataifa

Aliyesomeshwa na mchumba aamuriwa kurudisha Sh 9.4 Mil. baada ya kukataa kuolewa

Spread the love  MWANAMKE mmoja nchini Uganda ambaye aliuumiza moyo wa mchumba...

Habari

Mnyika aacha ujumbe msibani kwa kada wa Chadema aliyefia vitani Ukraine

Spread the loveKATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo-Chadema Taifa, John...

HabariHabari Mchanganyiko

Mwili wa kada wa Chadema aliyefia vitani Ukraine wawasili, kuzikwa Mbeya

Spread the loveMWILI wa Kada wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo-Chadema, aliyefia...

error: Content is protected !!