November 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mke aliyeachwa na mumewe achoma nyumba, apandishwa kizimbani

Spread the love

 

MWANAMKE mmoja raia wa Kenya amepandishwa kizimbani kwa tuhuma za kuchoma moto nyumba ya mumewe waliyetengana naye na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh milioni 100.2. Anaripoti Mwandishi Wetu (endelea)

Mwanamke huyo aliyefahamika kwa jina la Esther Mummy Webisa (37) alifikishwa mbele ya Hakimu Mwandamizi, Derrick Kutto kwa kuteketeza nyumba ya mumewe iliyopo katika mtaa wa Akiba eneo la South C jijini Nairobi.

Pamoja na kuchoma nyumba ya mumewe aliyefahamika kwa jina la Fulgence Gaspe Assenga pia moto ulisambaa na kuchoma nyumba ya jirani yake Stella Mkafitina.

Esther ambaye sasa anakabiliwa na shtaka la kuchoma nyumba mbili za makazi, alikana kuchoma moto nyumba hizo zenye thamani ya Sh milioni 100.2

Akijitetea mbele ya hakimu huyo, Esther alidai kuwa tarehe 28 Oktoba mwaka huu alisafiri kutoka Bungoma kuelekea Nairobi kumtembelea mumewe waliyetengana lakini alipofika hakufunguliwa geti na hata majirani walipomshauri ampigie simu mumewe haikupokewa ndipo alipoamua kuruka ukuta na kuingia ndani.

Aidha, mlalamikaji wa kwanza yaani mumewe alidai mkewe huyo waliyetengana, alipoingia ndani alizua varangati na kumuumiza mkono.

Alidai aliamua kwenda kuripoti tukio hilo polisi kabla ya kupata matibabu lakini akiwa kituoni kuandikisha maelezo alitumiwa ujumbe mfupi wa maneno kwenye simu yake kuwa nyumba yake inaungua.

Maofisa wa polisi na maofisa wa idara ya wazima moto ya kaunti ya Nairobi waliuzima moto huo  kisha kumkamata Esther.

Aidha, mlalamika wa pili ambaye ndiye jirani ambaye nyumba yake iliungua, aliieleza mahakama karibu na yeye ateketee kwa moto ndani yake kwani aliokolewa na majirani.

Hata hivyo, Esther aliachiliwa kwa dhamana ya Sh milioni 20.5 huku kesi hiyo ikitarajiwa kutajwa tena tarehe 18 Novemba mwaka huu.

error: Content is protected !!