OFISI ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), imemburuza Wakili Boniface Mwabukusi, mbele ya Kamati ya Maadili ya Mawakili, ikimtuhumu kwa makosa ya ukiukwaji wa maadili, wakati akishughulikia sakata la mkataba wa uendeshaji bandari ulioingia kati ya Serikali ya Tanzania na Imarati ya Dubai. Anaripoti Mwandishi Wetu, Dar es Salaam…(endelea).
Ofisi hiyo imewasilisha malalamiko katika kamati hiyo, ikitaka Wakili Mwabukusi avuliwe uwakili kwa madai kwamba amekiuka maadili ya taaluma ya uwakili.
Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa tarehe 20 Novemba 2023 na Wakili Alphonce Lusako, ambaye ni miongoni mwa jopo la mawakili tisa wanaomtetea Wakili Mwabukusi, kesi hiyo inasikilizwa leo Jumatatu hadi kesho Jumanne.
Wakili Lusako amedai kuwa, kesi hiyo imeanza kusikilizwa leo kuanzia saa 4.00 asubuhi na kwamba kesho ikimalizika, kamati hiyo itatoa tarehe ya uamuzi.
Hata hivyo, Wakili Lusako anadai, jopo la mawakili hao wa utetezi linaloongozwa na Wakili mwandamizi, Mpare Mpoki, limeweka mapingamizi ya awali dhidi ya hoja zilizowasilishwa na AG, wakiiomba kamati hiyo izitupilie mbali kwa madai kuwa hazina mashiko.
“Ni kweli Wakili Mwabukusi anashtakiwa kwa makosa kadhaa kwamba amekiuka maadili ya uwakili wakati ule wa kesi ya bandari, sasa wanamtuhumu kwa tuhuma kadhaa kwamba alidanganya, alivyozungumza kwamba spika wa bunge na waziri mkuu hawajui wanachopitisha bungeni kama mkataba au makubaliano,” amedai Wakili Lusako.

Mbali na Wakili Mpoki, mawakili wengine waliojitokeza kumtetea Wakili Mwabukusi ni pamoja na, Wakili Edson Kilatu, Dk. Rugemeleza Nshalla, Tito Magoti, Emmanuel Chengula na Dickson Matata.
Mtandao umezungumza na Wakili Mwabukusi kwa njia ya mtandao wa WhatsApp, ambaye amekiri kufikishwa mbele ya kamati hiyo na kwamba kwa sasa shauri hilo linaendelea kusikilizwa.
Kwa mujibu wa barua ya wito kwenda kwa Wakili Mwabukusi, iliyosaniwa Julai 2023 na Katibu wa Kamati ya Maadili ya Mawakili, Faraji Ngukah, AG anamtuhumu mwanasheria huyo kwa kukiuka maadili ya uwakili kutokana na kutoa kauli za uchochezi.
Miongoni mwa kauli zinazolalamikiwa na AG, ni ile ambayo Wakili Mwabukusi alimtuhumu Spika wa Bunge, Dk. Tulia Ackson na Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, kwamba hawajui walichokipitisha bungeni.
“Spika wa Bunge, waziri mkuu hawajui walichokipitisha bungeni, kwamba hata chifu Mangungo anasingiziwa maana yeye alijua kuwa ni mkataba….Serikali imekuwa ikiwadanganya wananchi kuwa imesaini makubaliano na siyo mkataba,” kauli iliyonukuliwa na AG katika malalamiko yake dhidi ya Wakili Mwbaukusi.
Kauli nyingine zinazodaiwa kutolewa na Wakili Mwabukusi ambazo AG anailalamikia ni “Bunge kwa makusudi liliamua kusimamisha akili zake, utashi wake na uadilifu wake kwa mahaba ya mtu na wakasema mkataba huu ni wa mtu na kupitia mkataba huu, yeyote atakayeupinga ni adui wa mtu huyo.”
Pia, AG anamtuhumu Wakili Mwabukusi kwa kutoa kauli zenye lengo la kupunguza uaminifu wa wananchi dhidi ya mfumo wa mahakama.
Leave a comment