January 28, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mkanganyiko CCM Z’bar

Spread the love

CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimeingia tena katika mvutano na wanachama wake waliokabidhiwa vyeti vya ushindi wa uwakilishi na udiwani katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 25 mwaka jana, kwa kushikilia kuwa hawataki uchaguzi wa marudio, anaandika Jabir Idrissa.

Baadhi ya wawakilishi wamesema hawaoni sababu ya msingi ya chama kujiingiza katika uchaguzi mwingine wakati wanachama wake walishatangazwa washindi baada ya kuchaguliwa na wananchi.

“Kwa mfano mimi binafsi nimetangazwa mshindi wa kiti cha uwakilishi jimboni kwangu. Nina cheti nilichokabidhiwa na msimamizi wa uchaguzi wa jimbo, sasa inaingia akilini kweli kuniingiza kwenye uchaguzi mwingine?”

Mwakilishi huyo ambaye kwa sababu za kuhofia kuchukuliwa hatua za kinidhamu na chama hataki kutajwa kwa jina, amesema kuna shida ndani ya akili za viongozi wa CCM ambazo zinasababisha kuingiza nchi kwenye mgogoro mkubwa wa kikatiba na kisiasa.

“Huwezi kuamini viongozi wetu wanashikilia uchaguzi wa marudio ilhali wanajua kwamba hakuna haki ya kuwaingiza wananchi kwenye uchaguzi mwingine kwa kuwa uliofanyika Oktoba na kupatikana washindi haukuwa na matatizo,” amesema.

Alipoulizwa kama wana mshikamano katika msimamo wake kwa maana ya wawakilishi wenzake wanafikira kama yeye, mwakilishi huyo amesema “sote tunazungumzia suala hili tangu siku zile za mwanzo baada ya uchaguzi kufutwa, lakini tatizo ni viongozi wetu wachache wa juu kufikiria zaidi maslahi binafsi kuliko ya nchi.”

Mwakilishi huyo wa moja ya majimbo ya Wilaya ya Mjini, anapozungumza hayo, kunakuja taarifa kutoka ndani ya CCM kuwa hata baadhi ya wajumbe wa Kamati Maalum ya Halmashauri Kuu ya Taifa Zanzibar hawaafiki uchaguzi wa marudio.

“Nakwambia tunapinga suala hili lakini wachache wanalishikilia kama vile lina maana yoyote kwa maslahi ya nchi na watu wake. Wapo viongozi wakubwa wanadhani wana haki ya kuungwa mkono kwa kila wanachokiamini wao, kumbe wanachokipigania ni maslahi binafsi ndani ya utashi wa kujenga siasa za chuki nchini. Tufike mahali mtindo huu ukome ili kuipa nchi nafasi ya kusonga mbele kama wenzetu,” amesema.

Kwa mujibu wa taarifa, kamati maalum ilifanya kikao katikati ya wiki iliyopita mjini Zanzibar na kujadili uchaguzi wa marudio lakini idadi kubwa ya wajumbe walipinga uchaguzi huo.

Taarifa zinasema wajumbe 35 walipiga kura ya kukataa uchaguzi wa marudio, tisa waliridhia na wengine walikataa hata kupiga kura. “Baadhi ya wajumbe waliamua kutoka nje ya ukumbi kwa kuchukizwa na chagizo za viongozi wakubwa wachache kulazimisha uchaguzi wa marudio,” amesema mwanamama kutoka Mkoa wa Kaskazini Unguja.

Pamoja na CCM kushikilia kuendeshwa uchaguzi wa marudio Machi 20, bado wanavutana kwa kila kukicha kuendeleza vikao vya mikakati wakati dunia nzima inaishangaa Zanzibar kwa kujiingiza katika utaratibu wa kukandamiza maamuzi ya wananchi waliochagua kwa utulivu mpaka Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kutangaza matokeo ya majimbo 31 ya urais na kukamilisha kazi ya kuhakiki kura za majimbo tisa mengine.

error: Content is protected !!