MWENYEKITI wa Kamati ya Mipango Miji katika Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Amir Nondo ameiomba iundwe kamati maalum kwa ajili ya kusimamia barabara ya Mei Mosi kwa kuwa ujenzi wake umeshindwa kukamilika. anaandika Christina Haule.
Nondo alisema hayo jana kwenye kikao cha kawaida cha baraza hilo ambapo ameliambia kwamba Mkandarasi anayejenga barabara hiyo kampuni ya Jassie Company Ltd, Building and Civil Engineering Contractor na kampuni ya ushauri ya M/S Dosh Ltd kwa sasa wamekimbia hazi na hawa[o eneo la mradi.
Aidha, Nondo alisema, fedha za mradi huo zimetolewa Benki ya Dunia na kwamba kati ya fedha hizo zinaendelea kutumika katika kuboresha masuala mbalimbali ya kuleta maendeleo ya Manispaa.
Alisema ujenzi wa barabara hiyo ya Mei Mosi ulianza tangu Julai mosi 2015 ambapo ulitarajiwa kukamilika Julai 30, 2016, lakini mpaka sasa bado haujakamilika.
“Sisi tumepata mradi mkubwa ndani ya Halmashauri 18 Tanzania zilizoomba huku tukiwa tumepata fedha nyingi sasa doa hili tukilinyamazia litasababisha kukosa miradi mingine” alisema.
Amefafanua kwamba kamati hiyo itakuwa na uwezo wa kupima kazi hata kwa kushirikisha msaada wa taasisi zingine za ukaguzi na kuona kama kweli ujenzi huo umeenda sambamba na mkataba uliopo.
Kwa uapnde wake, Mstahiki Meya wa Halmashauri ya Manispaa ya Morogoro, Pascal Kihanga aliahidi kujadiliana na kamati ya ujenzi na mipango miji na kuona namna ya kuunda kamati hiyo.
Aidha, Kihanga alisema kuwa licha ya Mkandarasi huyo kutokuwepo kwenye eneo la mradi anaendelea kukatwa asilimia 10 ya hela yake kwa mwezi.
Kwa sasa alisema wamekusanya kiasi cha Sh. milioni 293.7 ambazo zimekusanywa kwa miezi saba na kuziweka kwenye akaunti ya Manispaa ambapo zitaingizwa kwenye shughuli zingine za maendeleo ya Manispaa hiyo kwa mujibu wa mradi wa Benki ya Dunia.
Naye Mbunge wa jimbo la Morogoro mjini, Abdulaziz Abood alisisitiza Halmashauri hiyo kuhakikisha fedha anazolipwa mkandarasi huyo zinaendana na kazi inayofanywa ili kuepuka hasara.
Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri hiyo, Michael Waruse alisema, fedha zinalipwa kwa mujibu wa sheria na mkataba uliopo na kwamba mkandarasi huyo hulipwa fedha kwa kazi anayoifanya.
Ujenzi wa barabara hiyo yenye urefu wa km 5.1 kwa kiwango cha lami unaogharimu Sh. bilioni 11,805,176,469.00 ulishindwa kukamilika kwa wakati na kufanya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Utawala Bora na Serikali za Mitaa kutoa mwezi mmoja kukamilisha kazi hiyo.
Leave a comment