May 20, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mkakati wasukwa kuwang’oa Mdee, wenzake

Susan Kiwanga, Mjumbe wa Kamati Kuu Chadema

Spread the love

 

MAKAKATI umeanza kusukwa ili kuhakikisha Halima Mdee na wenzake 18, wanang’olewa bungeni. Anaripoti Regina Mkonde, Dar es Salaam … (endelea).

Mkakati huo unasukwa na Baraza la Wanawake la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Bawacha), kupitia kamati tendaji zake ngazi ya majimbo.

Mbele ya waandishi wa babari leo Jumanne, tarehe 4 Mei 2021, jijini Dar es Salaam, Susan Kiwanga ambaye ni Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho amesema, makakati huo utaanza kusukwa hatua kwa hatua.

Kauli ya Kiwanga inatoka ikiwa ni siku moja baada ya Spika wa Bunge, Job Ndugai kusisitiza, wabunge hao wako bungeni kwa mujibu wa sheria na atawalinda.

Wabunge hao ni Halima Mdee, aliyekuwa Mwenyekiti wa Bawacha Taifa, Ester Bulaya, Esther Matiko, Grace Tendega, Hawa Mwaifunga, Agnesta Lambart, Asia Mohamed, Jesca Kishoa, Nusrat Hanje na Tunza Malapo.

Wengine ni Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.

Wabunge hao wakiongozwa na Mdee, walifukuzwa uanachama Novemba 2020, kwa tuhuma za usaliti kufuatia hatua yao ya kuapishwa kuwa wabunge viti maalum, kinyume na msimamo wa Chadema wa kutowasilisha wawakilishi wao bungeni, wakipinga matokeo ya Uchaguzi Mkuu.

“Tunazitaka Kamati za Utendaji Bawacha kukutana kila mkoa kujadili hatua za kuchukua kuhusu suala hili, kwa kuwa wanawake hatutakuwa tayari kuona mtu yeyote akivunja Katiba.”

“Baada ya kupata mapendekezo kutoka kwenye majimbo, tutachukua hatua kushinikiza utekelezwa wa jambo hili,” amesema Kiwanga.

Jana Jumatatu tarehe 3 Mei 2021, akiwa bungeni jijini Dodoma, Spika Ndugai alisema, yeye hajavunja Katiba ya nchi kufuatia hatua yake ya kuwapokea wabunge hao.

Kwa maelezo, kwamba hakupokea barua kutoka Chadema kuhusu sakata hilo, bali alipokea kipeperushi kisichokuwa na Katiba wala muhtasari wa kikao kilichowafukuza wabunge hao.

Akizungumzia kauli hiyo, Kiwanga amesema “sote tunatambua kwamba, mawasiliano rasmi kati ya taasisi na taaisisi ni kwa njia ya maandishi, ndiyo maana tulimuandikia barua kumueleza juu ya maamuzi yaliyofikiwa na kamati kuu kwa mujibu wa katiba ya Chadema.

Job Ndugai Spika wa Bunge la jamhuri ya muungano wa Tanzania

“Hata hivyo, baada ya kujibu barua ya katibu mkuu (John Mnyika), spika ameibuka miezi mitano baadae akazungumza bungeni ambapo si njia ramsi ya mawasiliano lakini pia hakuna kiongozi wa Chadema bungeni anamjibu nani kule bungeni?” Amehoji Kiwanga.

Kiwanga amesema, wanawake wa Bawacha wanamshauri Spika Ndugai afuate Katiba ya nchi ili kuleta usawa.

“Tunamtaka spika asijisifie miaka minganpi amekaa ndani ya bunge, aangalie kwenye kipindi cha uongozi wake ameacha alama gani kwenye nchi, alama zenye kuliunganisha taifa, kuleta amani, haki na usawa kwa wote huku ikiweka misingi kuheshimu katiba, sheria na taratibu mbalimbali tulizojiwekea,” amesema Kiwanga.

error: Content is protected !!