July 7, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mkakati wa UKAWA waiva

Viongozi wa Vyama vinavyounda Umoja wa wadai Katiba ya Wananchi (UKAWA) wakitiliana saini ya kukubaliana kuungana

Spread the love

VYAMA vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), viko kwenye hatua za mwisho za kuweka utaratibu wa pamoja kwa ajili ya kuwapata wagombea wake katika nafasi za urais, ubunge na udiwani katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu. Wanaandika Deusdedit Jovin na Pendo Omary… (endelea)

Hatua hizo zinachukuliwa ili kuondoa uwezekano wa migongano inayoweza kujitokeza wakati wa uteuzi wa wagombea katika nafasi hizo.

Akizungumza na MwanaHALISI Online, Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willibrod Slaa, amesema katika kukidhi matarajio ya Watanzania kuhusu nafasi ya UKAWA katika uchaguzi ujao, wataweka na kukubaliana kuhusu vigezo ambavyo vitatumika kumpata mgombea mmoja kwa kila nafasi ya uongozi.

“Vigezo viko vingi. Baadhi yake ni kigezo cha mtu kukubalika katika eneo husika, kuungwa mkono na vyama vyote vinavyounda UKAWA na nguvu ya chama katika eneo husika. Vigezo vingine bado tunavishughulikia,” amesema Dk. Slaa.

Naye Profesa Ibrahim Lipumba, Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), amesema kwamba iwapo kutatokea mgongano wa wagombea, zipo kamati za maamuzi ambazo zitashughulikia suala hilo.

“Ni wazi katika uchaguzi ujao kutakuwa na matatizo hayo. Lakini kamati zetu za maamuzi, ikiwemo pia kamati ya siasa, zitayashughulikia ipasavyo,” amesema Prof. Lipumba.

Ameongeza kwamba, kitendo cha vyama vya CUF na NCCR Mageuzi kuanza kutoa fomu za kuwania uongozi kwa wanachama wao, ni mchakato wa kawaida ndani ya vyama hivyo.

Hivyo, Prof. Lipumba anakanusha ‘propaganda’ kwamba kwa hatua hiyo wamejiondoa katika UKAWA.

MwanaHALISI Online ilimtafuta Dk. Emanuel Makaidi, Mwenyekiti wa Chama cha National League for Democracy (NLD), kuhusu ushiriki wa chama chake katika UKAWA kwa kuzingatia kwamba ana idadi ndogo ya viongozi waliochaguliwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka jana. Amesema “hilo sio tatizo”.

“Kutokana na kuwa na wajumbe wachache mimi ni junior partner (mshirika mdogo), lakini hiyo hainikatazi kushiriki kikamilifu sawa na wenzangu. Ushiriki wangu ndani ya UKAWA umesaidia kukuza chama changu kwa kuongezeka kwa wanachama tofauti na awali kabla ya kujiunga na UKAWA.

“Nafasi yangu ndani ya UKAWA ni muhimu sana. Mimi ni mzee kuliko wote. Hivyo ushauri wangu ndani ya umoja huo unazingatiwa sana,” amesema Dk. Makaidi.

Katika kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu, inatarajiwa kwamba uteuzi wa wagombea ndani ya UKAWA utakuwa na hatua mbili: uteuzi wa ndani ya kila chama na uteuzi katika ngazi ya UKAWA.

Uteuzi katika ngazi ya chama kimoja kimoja, utaongozwa na katiba ya chama husika wakati kwa upande wa UKAWA utaongozwa na taratibu zitakazokubaliwa na vyama vyote.

Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanasema kuwa, endapo taratibu hizo zitawekwa na kuzingatiwa ipasavyo, basi zitakuwa ni nyenzo muhimu katika harakati za kukifuta Chama Cha Mapinduzi (CCM) katika kudhibiti dola.

error: Content is protected !!