July 29, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mkakati wa Magufuli, Dk. Tulia ‘kuua’ Ukawa

Spread the love

 

MIKAKATI inayofanywa na Serikali ya Rais John Magufuli dhidi ya vyama vya upinzani nchini, inalenga kudhoofisha upinzani huo kabla ya uchaguzi mkuu 2020, anaandika Dany Tibason.

Miongoni mwa matukio yanayoakisi dhamira hiyo ni tukio la jana ambapo Freeman Mbowe, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema-Taifa), Patrobas Katambi, Mwenyekiti wa Bavicha na Julius Mwita, Katibu Mkuu Bavicha kukamatwa na polisi bila maelezo yaliyonyooka.

Wengine katika sekeseke hilo ni Frank Mwakanjoka, Mbunge wa Tunduma, viongozi wengine na baadhi ya wanachama.

Ingawa hakuna sababu zilizotolewa, huenda viongozi hao wameshikiliwa kwa makosa ya kusalimiana na wananchi kwani Mbowe jana alikuwa akipita kwa miguu kwenye baadhi ya vijiwe vya wananchi na kuongea nao mambo ya kawaida.

Mbowe na viongozi wenzake wapo jijini Mwanza wakisubiri hatma ya kesi waliyofungua, kupinga kuzuiwa mikutano yao ya hadhara.

Jijini Dar es Salaam, Zitto Kabwe, Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo na wafuasi wake jana walitimuliwa na polisi na kuzuiwa kufanya kongamano la ndani kwa madai ya usalama.

Lengo la mikakati hiyo ni kuvinyima nafasi vyama hivyo kufanya siasa ndani na nje ya Bunge hivyo kuviweka kwenye mazingira magumu ya ushindani kwenye uchaguzi mkuu ujao.

Mikakati hiyo inayofanywa kupitia vyombo vya dola, bungeni na nje ya Bunge imekuwa ikilenga vyama vyenye nguvu, hasa vile vinavyoundwa  na Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Ukawa unaundwa na vyama vya Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Chama cha Wananchi (CUF), NCCR Mageuzi na Chama cha NLD ambacho hata hivyo hakina nguvu kubwa na hakina uwakilishi bungeni.

Chama kingine ambacho kiko nje ya Ukawa na ambacho pia kimekuwa kikikumbana na dhahama ya vyombo vya dola ni ATC Wazalendo, kinachoongozwa na Zitto, Mbunge wa Kigoma Mjini.

Hivi karibuni Zitto alifanya mkutano wa hadhara katika Viwanja vya Mwembe Yanga, jijini Dar es Salaam, lakini siku iliyofuata aliitwa polisi na kuhojiwa kwa madai ya kutoa lucha chafu dhidi ya serikali.

Jana mbunge huyo na chama chake walikuwa na kungamano la ndani, lakini polisi walivamia na kuwatawanya viongozi na wafuasi wa chama hicho, ikiwa ni sehemu ya kuminya uhuru wa vyama vya siasa kujieleza mbele ya wananchi wake.

Duru za siasa zinaeleza kuwa, dalili za kutekeleza mkakati wa kuuwa vyama vya siasa zilianza kuonekana tangu serikali ya awamu ya tano chini ya Rais Magufuli ilipoingia madarakani.

Ikumbukwe kuwa, mwanzo mwa mwaka huu aliyekuwa mgombea urais wa Ukawa, Edward Lowassa (Chadema), kilipanga kufanya mikutano nchi nzima ya kuwashukuru wananchi kwa imani kubwa waliyoionesha kwa kuwapa kura madiwani, wabunge na kura nyingi za urais.

Lowassa alipata kukaririwa kwamba, anaamini alishinda uchaguzi huo na kudai kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ilichakachua kura zake na kumpa ushindi Dk. Magufuli.

Katika uchaguzi mkuu uliopita, Magufuli alishinda kwa kura 8, 882, 935 huku Lowassa akipata kura 6, 072, 848.

Licha ya kushindwa, Lowassa alisema atazunguka nchi nzima kuwashukuru wananchi na kuwaeleza ukweli kilichotokea hadi akashindwa.

Baada ya kutangaza hivyo, siku chache baadaye akiwa mkoani Lindi, Kassim Majaliwa, Waziri Mkuu alitangaza kupiga marufuku mikutano yote ya hadhara ya vyama vya siasa kwa madai kuwa, hali ya kisiasa nchini baada ya uchaguzi sio shwari.

Lakini Waziri Majaliwa alipobanwa bungeni, alisema hajazuia mikutano ya hadhara kwa nchi nzima kwani zuio lake lililenga katika jimbo lake tu.

Kana kwamba hiyo haitoshi, mkakati wa kushughulika na wapinzani ulihamia bungeni pale Bunge lilipozuia kurushwa kwa matangazo ya kipindi cha Bunge moja kwa moja (Live).

Ingawa serikali awali ilidai kufanya hivyo kutokana na ukosefu wa fedha, lakini uchunguzi ulibaini kuwa hatua hiyo ililenga kuwathibiti wapinzani.

Ni kwa madai kuwa, wamekuwa wakitumia Bunge kujipatia umaarufu na wakati mwingine kusababisha serikali kutikisika kwani zaidi ya mawaziri 15 katika serikali zilizopita waling’olewa kwa hoja zilizoibuliwa na wapinzani Bungeni.

Katika kutimiza mkakati huo wa kuua wapinzani, Bunge limekuwa chombo muhimu kuendesha mkakati wa kupambana na kuwadhibiti wapinzani.

Ndani ya Bunge, mkakati huo unaendeshwa na Dk. Tulia Ackson, Naibu Spika wa Bunge kiasi kwamba Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imetangaza na inatekeleza msimamo wake wa kususia vikao vyote vinavyoendeshwa na Naibu Spika huyo kwa madai kuwa, hawana imani naye.

Wabunge hao wa Ukawa wamedai wataendelea kumsusia kwani anaendesha  Bunge kibabe na hali hiyo imesababisha baadhi ya wabunge kusimamishwa kuhudhuria vikao na mikutano kadhaa ya Bunge.

Wabunge waliokwishaadhibiwa kwa kufungiwa kuingia bungeni hadi sasa ni Zitto Kabwe (Kigoma Mjini), Halima Mdee (Kawe), Tundu Lissu (Singida Mashariki), Godbless Lema (Arusha Mjini), John Heche  na Esther Bulaya (Bunda).

Kuna uwezekano wa wabunge wengine wa upinzani kufungiwa kwani hivi karibuni Dk. Tulia  aliagiza Kamati ya Haki, Kinga na Maadili ya Bunge, kumhoji Joseph Mbilinyi (Sugu), Mbunge wa Mbeya Mjini-Chadema, kwa madai ya kuonesha kidole cha kati juu wakati akitoka nje ya ukumbi wa Bunge, ishara ambayo imetafsiriwa kama matuzi na dharau kwa Kiti cha Spika.

Agizo la kuzuia mikutano lililotolewa na Jeshi la Polisi, lilitokea siku moja baada ya wabunge wa Chadema waliotimuliwa bungeni na viongozi wao wa juu, kupigwa mabomu ya machozi, kumwagiwa maji ya kuwashwa kwenye mkutano wa hadhara uliopangwa kufanyika wilayani Bunda hivi karibuni.

Katika tukio hilo, wafuasi wengi wa Chadema walijeruhiwa na wengine zaidi ya 20 walikamatwa na kufikishwa mahakamani kwa madai ya kufanya mkutano uliozuiwa  na polisi.

 

error: Content is protected !!