January 23, 2022

Uhuru hauna Mipaka

Mkakati wa Magereza kupanua uzalishaji kiwanda cha sabuni Ruanda

Bidhaa zitokanazo na mti wa mwanzi ambazo zinazalishwa kiwandani hapo.

Bidhaa zitokanazo na mti wa mwanzi ambazo zinazalishwa kiwandani hapo.

Spread the love

“TUKIPATA mtaji wa Sh. milioni 500 badala ya 200 tunazopata sasa, tunaweza kukidhi malengo yetu. Kiwanda hiki kilianzishwa mwaka 1978 na sasa ndicho pekee kimebakia kati ya viwanda vya sabuni mkoani Mbeya. Vingine vyote zaidi ya vitatu vimekufa.

Kwa sasa mitambo yetu ni chakavu- ina uwezo wa kuzalisha kati ya katoni 100 mpaka 200 kwa siku lakini kimsingi lengo letu ni kuzalisha katoni 500 za sabuni za miche kwa siku.

Hii ndiyo ndoto aliyonayo Mkuu wa Kiwanda cha sabuni Ruanda mkoani Mbeya, Mrakibu wa Magereza, Huruma Mwalyage, alipotembelewa na waandishi wa habari kuona namna kiwanda hicho kinavyotekeleza program ya urekebishaji, kupitia miradi ya Magereza.

Mwalyage anaamini uwezo wa kufanya hivyo wanao kwa sababu wanayo nguvu kazi ya rasilimali watu ya kutosha. Anasema mradi huo ni miongoni mwa miradi 23 iliyoko chini ya Shirika la Magereza.

Lengo kubwa la mradi ni kutimiza majukumu ya msingi ya Jeshi la Magereza ambayo ni urekebishaji kwa wafungwa na pia kufanya biashara kupitia bidhaa zinazotengenezwa.

Mradi huu unajishughulisha na utengenezaji wa sabuni za aina tatu-za miche, dawa na kuogea na za maji. Sabuni za miche ziko za miche mifupi na minene maarufu kama sabuni za magadi, sabuni zenye miche minene na mirefu, zenye miche mirefu myembamba (magesafi).

Sabuni za kuogea, zipo zenye dawa maalum ya mimea (tiba soap) na vile vile wanatengeneza sabuni za maji kwa ajili ya kudekia na sabuni za unga.

Mwalyege anafafanua kuwa, “katika kujiongezea kipato mradi pia ulibuni vyanzo vingine vya kuongeza mapato ya mradi kwa kuanzisha utekelezaji wa bidhaa mbalimbali zinazotokana na malighafi ya mianzi, ushonaji wa vikapu vinavyotumia nyuzi za mkonge na pia shughuli za useremala”.

Hapa kupitia useremala wanatengeneza vitanda, meza, stuli, kabati za vitabu na kabati za kuwekea vitu mbalimbali.

Mwalyege anasema wafungwa anaowatumia katika mradi huo ni wenye vifungo vya kuanzia miaka 15 hadi 30 ambapo kila siku kiwanda kinakuwa na wafungwa wasiopungu 57.

Kuhushu malighafi zitumikazo kiwandani, anasema ni caustic soda ambayo huagizwa kutoka nje ya nchi, lakini kwa sabuni-malighafi zitumikazo hupatikana wilayani Kyela abazo ni mafuta ya Mise na Mawese.

“Kwa vifaa vya mianzi-malighafi hupatikana kutoka katika misitu ya Igoma na Santilya Mbeya vijijini. Malighafi zingine ni mbao kwa upande wa samani na blue na grease,”anasema.

Aliulizwa kuhusu soko la bidhaa zao, anasema nyingi hununuliwa kwa ajili ya matumizi ya wafungwa na kwa soko la nje kupitia maonesho ya kimataifa ya sabasaba na nanenane na pia kupitia tovuti ya Magereza bidhaa hizo zimekuwa zikipata wateja.

“Mbali na hilo pia sabuni hizo zinatumiwa sana na watu wa hapa Mbeya na pia maeneo ya karibu kama Iringa wananunua na kwenda kuuza kwa reja reja kwa sababu zinapendwa sana,” alisema Mwalyaje.

Anasema sabuni zilizowekwa dawa Magereza huzichukua kwa ajili ya kuwapatia wafungwa ziwasaidie kutunza ngozi dhidi ya magonjwa ya ngozi kutokana na msongamano wa wafungwa magerezani.

Mwalyaje anasifu juhudi za Kamishna Jenerali wa Magereza nchini, John Minja za kukifufua kiwanda hicho ambacho kilikuwa kimeanza kusua sua. Anasema

“Kamishna Minja amefanya jitihada kubwa za kukiwezesha kiwanda kupata vifaa na malighafi za utengenezaji sabuni, hivyo kukifanya kizalishe sabuni za kutosha kwa wafungwa waliopo magerezani pamoja na kukidhi soko mkoani Mbeya”.

Mradi huu ulianzishwa ili kutimiza majukumu ya msingi ya Jeshi la Magereza hasa utekelezaji wa programu ya urekebishaji wa wafungwa kwa kuwapatia ujuzi wa utengenezaji vitu mbalimbali ili pindi wamalizapo vifungo waweze kujiajiri au kuajirika wasirudie uhalifu.

error: Content is protected !!