October 26, 2021

Uhuru hauna Mipaka

Mkakati wa kumfukuza Lowassa CCM waiva

Viongozi wa CCM wakiongoza Mkutano wa Kamati Kuu ya CCM

Spread the love

MBUNGE wa Monduli, Edward Ngoyai Lowassa, aweza kuvuliwa uwanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), muda wowote kutoka sasa. Saed Kubenea, anaripoti.

Hoja ya kumvua uanachama Lowassa imepangwa kuwasilishwa katika kikao cha Kamati Kuu (CC), kinachotarajiwa kufanyika Jumanne wiki hii, mjini Zanzibar.

Taarifa kutoka ndani ya chama hicho zinasema, mkakati wa kumvua uwanachama Lowassa, unasukwa kwa ustadi mkubwa na baadhi ya viongozi wandamizi ndani ya CCM ili kumzua kutimiza ndoto yake ya kuwa rais.

“Ni lazima tumfukuze uanachama katika chama chetu. Hakuna namna nyingine ya kukinusuru chama hiki,” ameeleza kiongozi mmoja mwandamizi ndani ya chama hicho.

Amesema, “Bwana huyu (Lowassa), amekuwa akikivuruga chama chetu kwa muda mrefu. Tumemvulia, lakini sasa tumechoka. Nilazima tumuondoe ili kukinusuru chama chetu.”

Ajenda ya kumfukuza Lowassa kutoka ndani ya chama hicho, imejificha katika kinachoitwa, “Tathmini hali ya kisasa kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka huu.”

Lowassa alikuwa waziri mkuu wa kwanza katika serikali ya Jakaya Kikwete. Anatajwa kuwa miongoni mwa makumi ya wanachama wa CCM waliotangaza au kutajwa, kusaka urais kwa udi na uvumba katika uchaguzi mkuu ujao.

Januari mwaka jana, Lowassa na makada wenzake kadhaa walipewa “onyo” kwa kile kilichoitwa, “kuanza kampeni kabla ya muda kufika.”

Mtoa taarifa wa gazeti hili anasema, kabla ya kikao cha CC, kutafanyika kikao cha Kamati Ndogo ya Maadili na Nidhamu, ambacho kitafanya tathmini ya adhabu zilitolewa kwa Lowassa na wenzake.

Lowassa anatuhumiwa kuendelea na mkakati wake wa kampeni kwa kukusanya watu na kujipanga kwa ajili ya uchaguzi mkuu ujao, jambo ambalo viongozi wake wakuu wanamtuhumu kukipasua chama chao.

Anasema, kikao cha CC kitatekeleza mradi huo kwa kutumia ripoti zilizotengenezwa na timu za maofisa usalama wa chama hicho, zilizotumwa mikoa yote ili kukusanya kile kilichoitwa, “mkakati wa Lowassa wa kusaka urais.”

Kutokana na hali hiyo, Kamati Kuu iliitaka Kamati ya Maadili kufanya marejeo na kuangalia utekelezaji wa adhabu kwa makada hao sita.

Mtoa taarifa anasema, baada ya kikao cha Kamati ya Maadili kumalizika, kutawasilishwa kwa Rais Kikwete pendekezo la kumfukuza Lowassa kutoka katika chama hicho.

Mkutano wa Kamati Ndogo ya Maadili, utakuwa chini ya Makamu Mwenyekiti wa CCM (Bara), Philip Mangula.

Hata hivyo, wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanasema, kuna uwezekano mdogo mno kwa Kikwete kuweza kusimamia mradi huo hadi mwisho.

“Pamoja na mkakati huo kuendeshwa na viongozi wajuu wa CCM, lakini bado uwezekano wa kuutekeleza unakuwa mgumu. Hii ni kutokana na mwenyekiti Kikwete kuwa kigeugeu,” anaeleza kiongozi mmoja mwandamizi wa chama hicho.

error: Content is protected !!